Aibu ya paa kuvuja yalazimu Man U kuanza harakati za kuhama Old Trafford
MANCHESTER, UINGEREZA
WAMILIKI wa Manchester United wanatarajiwa kufanya uamuzi wa mwisho kuhusu kutumia zaidi ya Sh31 bilioni kujenga uwanja mpya wenye uwezo wa kubeba mashabiki 100,000 kabla ya mwisho wa mwaka 2024.
Sir Jim Ratcliffe ambaye ni mojwapo ya wamiliki wa United, anataka kujenga ‘Wembley ya kaskazini’ kwa timu hiyo, na kwa kushirikiana na Baraza la Trafford.
Ameteua jopo la kutathmini uwezekano wa uwanja mpya na kuboresha Old Trafford. Kikundi hicho kinajumuisha, Lord Sebastian Coe na kina wajumbe kama Meya wa Greater Manchester, Andy Burnham, na aliyekuwa nahodha wa ‘Mashetani Wekundi’ Gary Neville.
Vyanzo vya klabu vimehakikishia kuwa, jopo hilo limeshakutana mara nne, huku mijadala ikilenga zaidi kujenga uwanja mpya badala ya ukarabati wa uwanja uliopo, ambao ungegharimu karibu Pauni 1.2 bilioni na kuchukua muda mrefu kukamilisha.
Changamoto zimekuwepo katika kukarabati Old Trafford yenye uwezo wa kubeba mashabiki 74,310, ambayo imekuwa nyumbani kwa Manchester United tangu mwaka 1910.
Pia, reli iliyo nyuma ya sehemu ya mashabiki kuketi kwa jina Sir Bobby Charlton, inafanya iwe kazi ngumu kujenga uwanja katika sehemu hiyo.
Tofauti na Tottenham, ambao walicheza Wembley wakati uwanja wao ulikuwa unakamilishwa, United haina uwanja mbadala wa kutumia.
Ratcliffe anataka serikali za mitaa na kitaifa kushiriki katika kufadhili mradi mzima ingawa, kwa hali halisi, huenda ikawa kazi ngumu. Jinsi uwanja utakavyofadhiliwa ni moja ya mada zinazojadiliwa bado.
Vyanzo vimesema afisa mkuu wa operesheni wa United, Collette Roche, amekuwa akitathmini miradi ya kuboresha viwanja duniani kote, ikiwa ni pamoja na Uwanja wa Optus huko Perth, ambao ulifunguliwa mwaka 2018 na uwanja wa Bernabeu wa Real Madrid.
Pia kumekuwa na mazungumzo na maafisa kwenye Uwanja wa SoFi wenye uwezo wa 70,000, ambapo United ilishindwa na Arsenal katika mechi ya ziara ya Marekani Jumamosi.
Kuna uwezekano wakatumia uwanja huo wakisibiria wao kukamilika.
Klabu imeshauriana na mashabiki 30,000 kuhusu nini cha kufanya na inaamini kuna takriban mgawanyiko wa 50-50 wa kubaki au kuhama.
Ufadhili wa mradi huo bado unajadiliwa, kwa wazo la mchanganyiko wa ufadhili wa umma na wa kibinafsi.
United tayari imewasiliana na Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Keir Starmer, ambaye anasemekana yuko wazi kwa usaidizi wa serikali kuwasilisha usafiri kama sehemu ya mradi huo.