Dimba

Amorim adai mkosi ulichangia vijana wake Manchester United kupigwa na Aston Villa

Na MASHIRIKA December 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKUFUNZI wa Manchester United, Ruben Amorim, alionekana kukasirishwa na mkosi wa timu yake baada ya kichapo cha 2-1 dhidi ya Aston Villa Jumapili, katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Villa Park.

United walipata pigo kubwa katika mechi hiyo, baada ya nahodha Bruno Fernandes kupata jeraha na kumlazimisha Amorim kupanga upya safu yake ya kiungo baada ya mapumziko.

Morgan Rogers alifungia Villa mabao mawili dakika ya 45 na 57 nao Reds wakapata bao la kufutia machozi kupitia Matheus Cunha dakika za ziada za kipindi cha kwanza.

“Nadhani tulikuwa timu bora zaidi leo (Jumapili). Tulikuwa na bahati mbaya, hata kwa jeraha la Bruno, lakini wakati wa mchezo, hata bila yeye, tulikuwa timu bora zaidi,” Amorim alisema.

“Tulifanya kazi nzuri sana ambayo hakuna mtu atakayeikumbuka kesho, kwa sababu kinachojalisha ni matokeo.”

Amorim, 40, alisema Fernandes alionekana kuwa amepata jeraha la tishu laini na kwamba hajui atarejea lini.

Winga chipukizi Shea Lacey na kiungo Jack Fletcher walianza katika mechi hiyo.

“Tunahitaji kuwaandaa wachezaji wote tulio nao kwa mchezo unaofuata, hatuwezi kutumia chochote kama kisingizio. Hakuna mtu atakayekumbuka matatizo haya, kwa hivyo tukabiliane nayo. Itatufanya kuwa na nguvu,” Amorim alisema.

Beki wa United, Diogo Dalot, alikuwa mkweli katika tathmini yake ya kile ambacho alisema kuwa kumpoteza Fernandes kulimaanisha makubwa kwa upande wake.

United walishuka hadi nafasi ya saba na alama 26, 10 nyuma ya Villa iliyoganda nafasi ya tatu.

“Ni jambo kubwa. Hatujui ni mbaya kiasi gani, lakini kwake kutoka nje, tunajua jinsi alivyo wa maana katika kikosi chetu. Tunatumai, sio mbaya sana na tunaendelea naye kwa michezo inayofuata,” alisema.

Kama kawaida, kocha wa Villa Unai Emery alitoa tathmini ya mchezo na kukiri, alifurahishwa na ustahimilivu ulioonyeshwa na wachezaji wake.

“Nimefurahi sana,” alisema, “Wafuasi wetu wanapaswa kujivunia kila kitu tunachofanya pamoja kwa sababu nguvu ni muhimu sana. Jinsi wanavyotoa nguvu, jinsi wanavyotusaidia hapa kuhisi Villa Park ni ngome yetu.”