Dimba

Amorim kona mbaya Old Trafford klabu lejendari Wayne Rooney akimuita ‘limbukeni’

Na MASHIRIKA March 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MKUFUNZI wa Manchester United, Ruben Amorim, amejitetea baada ya nahodha wa zamani wa kikosi hicho, Wayne Rooney, kumuita kocha ‘mbichi na limbukeni’.

Matamshi ya Rooney yalichochewa na kauli ya Amorim kwamba lengo lake kuu ni kufufua makali ya miamba hao wa zamani na kuwaongoza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Man-United walipokezwa kichapo cha 10 kutokana na mechi 24 chini ya Amorim walipodenguliwa na Fulham kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya 1-1 mnamo Jumapili. Huo ni msururu wa matokeo duni zaidi ya Red Devils waliohitaji michuano 55 ili kupoteza 10 chini ya Erik ten Hag.

Ilikuwa mechi ya sita kwa Man-United kupoteza ugani Old Trafford tangu Amorim apokezwe mikoba ya ukufunzi mnamo Novemba, 2024.

Ilivyo, kushinda Europa League sasa ndiyo njia pekee iliyo halisi kwa Man-United kurejea kwenye mashindano ya bara Ulaya msimu ujao.

Hata hivyo, akihojiwa baada ya pambano hilo, Mreno huyo alizungumzia nia yake ya kuongoza Man-United kunyanyua taji la EPL kwa mara ya kwanza tangu 2013 Sir Alex Ferguson alipostaafu.

“Lengo letu kuu ni kushinda EPL. Najua tunasuasua na tunapoteza michuano lakini ndoto ingali hai. Sijui itachukua muda gani ila tutaendeleza azma hiyo na kusonga mbele pamoja hata iweje.”

Kwa mujibu wa Rooney, Amorim anapaswa kuzingatia zaidi malengo ya muda mfupi kama vile kuimarisha nafasi ya Man-United kwenye msimamo wa jedwali la EPL ndipo adumishwe kazini badala ya kuwapa mashabiki matumaini ya uongo.

“Nadhani ni ulimbukeni uliomsukuma kutamka kwamba wanawania taji la EPL kwa sababu hapo walipo kwa sasa ni mbali sana. Hata sidhani wameanza kunusia ubingwa wenyewe.”

Maoni ya Rooney kuhusu hali ya Man-United kwa sasa yana uzito mkubwa ikizingatiwa mafanikio yake katika klabu hiyo.

Anasalia kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa miamba hao na alishinda Kombe la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na mataji matano ya EPL akiwa tegemeo kuu la kikosi bora kilichonolewa mwisho na Ferguson.

Hata hivyo, ana rekodi mbovu ya ukufunzi, mwanzoni akifanya vyema licha ya hali ngumu huko Derby County kabla ya kuhamia Major League Soccer (MLS) kudhibiti mikoba ya DC United kisha kusimamia mechi 15 na 25 pekee kambini mwa Birmingham City na Plymouth Argyle.

Ingawa Amorim, 40, amekiri kuwa kibarua chake ugani Old Trafford ni “kigumu sana”, kubanduliwa kwa waajiri wake katika raundi ya tano ya Kombe la FA wakiwa mabingwa watetezi kuliendeleza masaibu yake na kuning’iniza pembamba hatima yake kambini mwa Man-United.

Hata katika EPL, Man-United wameshindwa mara 12 kutokana na michuano 27 iliyopita (W9, D6), hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi ya mechi ambazo wamepoteza kutokana na 27 za mwanzo wa msimu tangu 1973-74 (13), walipoteremshwa ngazi mara ya mwisho katika EPL.

Ushindi wa Fulham dhidi ya Man-United uliwarejeshea kumbukumbu za 1975 ambapo ni mara yao ya mwisho kufuzu kwa fainali ya Kombe la FA.

Shujaa wao mnamo Jumapili alikuwa kipa wa zamani wa Arsenal, Bernd Leno, aliyepangua penalti za Victor Lindelof na Joshua Zirkzee.

Chini ya kocha Marco Silva, Fulham sasa watakuwa wenyeji wa Crystal Palace kwenye robo-fainali za Kombe la FA huku Brighton wakiwa nyumbani dhidi ya Nottingham Forest au Ipswich.

Bournemouth watachuana na Manchester City uwanjani Vitality huku Preston, kikosi cha pekee kisichokuwa cha EPL ambacho kimesalia katika Kombe la FA, wakiwa wenyeji wa Aston Villa.

Mbali na Man-City waliotawazwa wafalme mnamo 2023, Ipswich ndio washindi wa hivi karibuni zaidi wa Kombe FA (1978) ambao wamesalia kwenye kivumbi hicho msimu huu. Fulham, Palace, Bournemouth na Brighton hawajawahi kuonja uhondo wa kulitwaa taji hilo.

Mechi za robo-fainali zitatandazwa wikendi ya Machi 29, 2025.

DROO YA ROBO-FAINALI ZA KOMBE LA FA:

Fulham vs Crystal Palace

Preston vs Aston Villa

Bournemouth vs Manchester City

Brighton vs Forest au Ipswich