Dimba

Arsenal walivyopata taabu mikononi mwa Aston Villa inayonolewa na kocha wao wa zamani

Na GEOFFREY ANENE December 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

LONDON, UINGEREZA

EMILIANO Buendia alifungia Aston Villa bao la ushindi dhidi ya Arsenal katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kuchangamsha mbio za kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Ushindi huu ulikuwa wa sita mfululizo nyumbani kwa vijana hao wa kocha Unai Emery na umewapa motisha ya kuwa miongoni mwa vikosi vinavyowinda kombe la EPL msimu huu.

Kufuatia ushindi huo Villa walipanda hadi nafasi ya pili na alama 30 nyuma ya Arsenal, ambao sasa wamewaacha na pengo la pointi tatu pekee baada ya kila mmoja kucheza mechi 15.

Wenyeji walitangulia kufunga kupitia kwa Matty Cash dakika ya 36 kabla ya Leandro Trassard kusawazisha dakika ya 52.

Mechi za EPL zitaendelea leo ambapo Brighton itaalika West Ham United jioni nao Fulham wakabiliane na Crystal Palace usiku.

Hapo kesho wavuta-mkia Wolves watakuwa wenyeji wa Manchester United uwanjani Molineux usiku.

Wolves wamepewa asilimia 25 ya kuandikisha ushindi wao wa kwanza msimu huu kulingana na ubashiri wa kompyuta ya Opta, nao United wamepewa asilimia 51.2% kuondoka na ushindi.

Licha ya kushindwa katika mkondo wa pili na wapinzani wao msimu uliopita, Man United hawajawahi kushindwa mara mbili mfululizo na Wolves ugani Molineux tangu Agosti 1980.

Wolves imedorora msimu huu ikipata pointi mbili pekee katika mechi 14.

Vijana hao wa kocha Rob Edwards bado wanasaka ushindi wao wa kwanza tangu msimu uanze; wamechapwa mechi 12 na kutoka sare mbili, huu ukiwa moja ya misimu mibaya zaidi kwenye historia yao.

Wolves wamewahi tu kupoteza mechi nane mfululizo – kati ya Desemba 1981 na Februari 1982.