Dimba

Arsenal watoa onyo kwa wapinzani baada ya kulazimisha ushindi dhidi ya Newcastle

Na TOTO AREGE, MASHIRIKA September 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ARSENAL ilitoka nyuma Jumapili na kulazimisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Newcastle, katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Ugani St James Park.

Wenyeji walicheka na wavu wa kwanza dakika ya 34 kupitia mshambuliaji Nick Woltemade kabla ya Arsenal kusawazisha dakika ya 84 kupitia kiungo Mikel Merino.

Kiungo Gabriel Magalhaes alifunga bao la ushindi dakika ya nyongeza ya 96 na kuwapa Arsenal ya Mikel Arteta alama zote tatu na kupunguza mwanya wa alama kuwa mbili kwenye jedwali.

Awali, mechi hiyo ilionekana kama itaishia sare ya 1-1.

Baada ya ushindi huo sasa, walipanda hadi nafasi ya pili na alama 13 baada ya mechi sita.

Alama mbili nyuma ya vinara wa ligi na mabingwa watetezi Liverpool ambao walilala mikononi mwa Crystal Palace kwa kupoteza 2-1 Jumamosi.

Hata hivyo, ushindi huo sasa unatuma onyo kwa wapinzani baada ya Arsenal kushutumiwa na wengi kwa kukosa kunyakua taji misimu mitatu mtawalia.

Newcastle walikuwa wameifunga Arsenal huko St James’ Park katika mechi zao tatu zilizopita kwenye uwanja huo, huku Wanabunduki wakishindwa kufunga bao hata moja katika mechi hizo.

Mabao yote mawili ya Arsenal dhidi ya Newcastle yalikuwa kutoka kwa kona, na yalikuwa mabao yao ya 35 na 36 kutoka kwa hali kama hizo kwenye ligi tangu mwanzo wa msimu wa 2023/24, ambayo ni 15 zaidi ya timu nyingine yoyote katika kipindi hicho.

Aidha, Arsenal haiwezi kuendelea kutegemea mipira ya frikiki kama njia ya kufunga mabao.

Hawakuonyesha makali yao katika ushambuliaji dhidi ya Liverpool mwishoni mwa Agosti walipopoteza 1-0 – na lazima waboreshe uchezaji wao, wachanganuzi wa soka wanasema.

Katika mechi nyingine Jumapili, Aston Villa pia walitoka nyuma na kulazimisha ushindi wa 3-1 dhidi ya Fulham Ugani Villa Park.

Bao pekee la Fulham lilifungwa na Raul Jimenez dakika ya tatu nayo mabao ya Villa yakatiwa kimiani na Ollie Watkins, John McGinn na Emi Buendia dakika ya 37, 49 na 51 mtawalia.

Hata baada ya ushindi huo, Villa walisalia nafasi ya 16 na alama sita nao Fulham wakiwa nafasi ya 10 na alama nane.