Dimba

Arsenal yaacha maswali kuliko majibu kwa jinsi ilinusurika dhidi ya wanyonge Wolves

December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, Uingereza

ARSENAL waliendelea kukaa kileleni mwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuponea katika ushindi wa 2–1 dhidi ya Wolves walioko mkiani ugani Emirates.

Hata hivyo, namna walivyopata ushindi huo imeacha maswali mengi kuliko majibu kuhusu uwezo wao wa kutwaa ubingwa msimu huu.

Kile kilichotarajiwa kuwa mtihani rahisi nyumbani kiligeuka kuwa mechi ya wasiwasi na presha kubwa iliyoonyesha mapungufu yanayohitaji kuangaliwa kwa makini.

Arsenal walikuwa na umilikaji mkubwa wa mpira, lakini walishindwa kabisa kuvunja ngome ya ulinzi wa Wolves, hadi wakakosa hata shuti moja lililolenga lango katika kipindi cha kwanza, ikiwa ni mara ya kwanza msimu huu kwao kufanya hivyo kwenye mchuano wa ligi.

Kwa upande mwingine, Wolves walionekana kuwa hatari zaidi kabla ya mapumziko, wakitengeneza nafasi bora kupitia Hwang Hee-chan na Jorgen Strand Larsen, lakini wakazimwa na kipa David Raya pamoja na ulinzi wa mwisho wa Arsenal.

Kama ambavyo imekuwa mara nyingi msimu huu, bao la Arsenal hatimaye lilitokana na mpira wa ikabu badala ya mashambulizi yaliyojengwa kwa mtiririko mzuri.

Kona safi ya Bukayo Saka dakika ya 70 iligonga nguzo, ikamgonga mngogoni kipa wa Wolves Sam Johnstone na kisha ikaingia wavuni—ikiweka wazi utegemezi mkubwa wa Arsenal kwenye mipira ya ikabu.

Hata hivyo, drama ya dakika za mwisho ilizua hofu kubwa zaidi.

Wakati ushindi ulipoonekana kuwa karibu, Arsenal walilegea.

Dakika ya 90, mchezaji wa akiba Tolu Arokodare alifunga kwa kichwa bao lake la kwanza Ligi Kuu, na kunyamazisha Emirates, akiadhibu kile ambacho baadaye Mikel Arteta alikiita tabia za ulinzi “za kupooza” na “zisizokubalika”.

Arsenal waliokolewa kwenye muda wa nyongeza pale Yerson Mosquera alipopachika bao la kujifunga chini ya presha ya Gabriel Jesus, jambo lililookoa aibu ya viongozi hao na kuwapa pointi tatu ambazo, kwa haki ya mchezo, hawakustahili kabisa.

Ushindi huo umefikisha Arsenal pointi 36 na kudumisha pengo lao kileleni, lakini kuhitaji mabao mawili ya kujifunga kutoka kwa Wolves ili kuwafunga timu ambayo haijashinda mipepetano 16 mfululizo si ishara ya wazi ya mabingwa watarajiwa.

Arteta hakuficha hisia zake baada ya mechi, akilenga zaidi kushuka kwa viwango vya kikosi chake kuliko kupongeza uthabiti wao.

Arsenal walipata njia ya kushinda, kama wafanyavyo mara nyingi wapambaniaji wa ubingwa, lakini maonyesho kama haya yataendelea kuibua mashaka kama kweli wana kila kinachohitajika kwenda hadi mwisho.