Arsenal yaambiwa Gyokeres ni Sh10b
ARSENAL imeambiwa ilipe Sh10.2 bilioni ili kumpata straika matata Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27 yuko kwenye orodha ya mastraika watatu wanaowindwa na Arsenal.
Nyota huyo ambaye amevutia timu nyingi barani Ulaya kutokana na kiwango chake kizuri, mbali na kufunga mabao mengi, huenda akalipwa zaidi ya Sh34 milioni kwa wiki na kuwa miongoni mwa wanasoka wanaolipwa pesa nyingi katika kikosi hicho maarufu cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iwapo atakubali kuhamia Emirates.
Mchezaji huyo wa zamani wa Brighton na klabu ya Coventry amefunga mabao 95 katika mechi 100.
Mbali na Arsenal, staa huyo vilevile anawindwa na Manchester United ambao ni mahasimu wakuu wa Arsenal, ingawa kuna uwezekano mkubwa wa raia huyo wa Sweden kujiunga na The Gunners.
Hata hivyo, lazima timu inayotaka huduma za straika huyo iweke mezani Sh10 bilioni kwanza.
Mbali na Gyokeres, The Gunners vile vile imeweka orodhani washambuliaji Alexander Isak wa Newcastle United na Benjamin Sesko wa RB Leipzig, huku kocha Mikel Arteta akisukumwa apate mmoja wao haraka iwezekanavyo kwa mandalizi ya mapema kwa ajili ya msimu ujao.
Kwa hao wote, Arteta amesemekana kuwa shabiki mkubwa wa Isak, huku kukiwa na madai kwamba Newcastle haitamuachilia hasa iwapo itafuzu kwa michuano ya UEFA Champions League.
Hadi sasa, Isak hajasaini mkataba mpya kuendelea kuchezea Newcastle United, huku akisisitiza kufanya hivyo baada ya msimu kumalizika, mbali na kulenga kusaidia klabu hiyo kushinda ubingwa wa Carabao Cup.
Arsenal wangempata Sesko mapema lakini raia huyo wa Slovenia aliamua kuongeza mkataba wake na RB Lepzig kwa mwaka mmoja.
Nyota huyo anayekaribia umri wa miaka 22 vilevile amevutia klabu maarufu barani Ulaya.
Kuna madai kwamba mkurugenzi mpya wa Arsenal, Andrea Berta anamuona Gyokeres kuwa bora kati ya washambuliaji hao wote.
Wachezaji wengine wanaotarajiwa kujiunga na Arsenal ni Martin Zubimendi wa Real Madrid, Nico Williams wa Athletic Bilbao na kipa Joan Garcia wa Espanyol, wote wa ligi ya LaLiga.
Kwingineko, huenda Jeremie Frimpong wa Bayer Leverkusen mwenye umri wa miaka 24 akajiunga na Liverpool kama beki wa kulia kuchukua nafasi ya Tent Alexander-Arnold anayetarajiwa kujiunga na Real Madrid mara tu msimu utakampomalizika.
Wakati huo huo, Nottingham Forest inapanga kusajili James McAtee, huku Manchester United ikimtaka Liam Delap na wengine watatu.