Dimba

Beldine Odemba atajwa kocha bora mwezi Oktoba

Na TOTO AREGE November 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KOCHA wa Harambee Starlets, Beldine Odemba ndiye kocha bora wa mwezi Oktoba.

Odemba alitangazwa jana na Chama cha Wanahabari wa Michezo Nchini (SJAK) wakishirikiana na kampuni ya kucheza kamari ya Betika.

Kocha huyo aliongoza Starlets kufuzu kwa michunao ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Kinadada  (WAFCON) 2026.

Starlets walijikatia tiketi baada ya kuinyoa Gambia 4-1 kwa jumla ya mabao, katika raundi ya pili na ya mwisho ya kufuzu dimba hilo, ambalo litaandaliwa nchini Morocco.

Kenya itarejea michuano hii baada ya miaka 10 mara ya mwisho Kenya ikishiriki mwaka 2016 nchini Cameroon kwa mara ya kwanza.

“Tulisubiri sana muda huu ufike. Ningependa sana kushukuru Betika kwa kiwakumbuka wachezaji wa kike na kazi ya yangu kama kocha. Wachezaji walionyesha njaa ya kutaka kufuzu WAFCON katika kila mechi, ” alisema Odemba.

Aliongezea akisema, “Haikuwa rahisi lakini tulijiamini na kuhakikisha kwamba tumerejesha Kenya katika WAFCON,”

Bi. Marya Wachira, Mtendaji Mkuu wa Masoko wa Betika ambaye hakuweza kuhudhuria hafla hiyo alisema;

“Hongera sana kwa kocha Odemba kwa mafanikio haya. Kujitolea kwako na uongozi wako haujawahamasisha tu bali pia umeleta fahari kwa taifa”

Odemba alipigiwa kura na Jopo la waandishi wa SJAK na kuwashinda, Kevin Wambua (Kocha wa raga wa Shujaa), Musa Benjamin (kocha wa ndondi wa Kenya), Nicholas Muyoti wa Nairobi United FC, Meshack Senge wa magongo, Simon Odongo (kocha wa raga wa Lionesses), na kocha wa taifa wa triathlon Camilla Lydya.

Mwenyekiti wa Jopo Abuller Ahmed, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Tendaji ya SJAK, kwa upande wake alibainisha kuwa,

“Ushindi wa kauli moja wa Kocha Odemba ni ushahidi wa uongozi wake bora na kujitolea kwake bila kuyumbayumba. Yeye ni bingwa wa kweli ambaye ameleta fahari kwa Kenya.”

Kocha huyo mwenye leseni ya ukufunzi ya A, alienda nyumbani na kikombe na hundi la Sh 100,000.