CHAN: Tanzania yajipa heshima nyumbani
TANZANIA ilianza kampeni ya kuwania ubingwa wa CHAN kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Burkina Faso ambao walipigiwa upatu wa kushinda katika pambano hilo la ufunguzi.
Abdul Suleiman alifunga penalti kipindi cha kwanza kikielekea kumalizika baada ya Clement Mzize kuangushwa kwenye eneo la hatari kabla ya Mohamed Hussein kuongeza bao la pili kwa kichwa katika dakika ya 70.
Bao hilo la pili lilihesabiwa baada ya ukaguzi wa VAR kwenye mechi hiyo ya Kundi B iliyochezewa katika uga wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Jumamosi usiku.
Mbele ya mashabiki wao wa nyumbani waliojitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hiyo, Taifa Stars ambao wanaorodheshwa katika nafasi ya 103 kwenye msimamo wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) waliumiliki mpira kwa kiasi kikubwa dhidi ya wapinzani wao ambao wanajivunia nafasi ya 63 kwenye orodha hiyo.
Mapema katika mechi hiyo, kipa Ladji Brahima Sanou wa Burkina Faso alifanya makosa ambayo karibu yaigharimu timu yake baada kushindwa kuzuia krosi.
Souleymane Sangare wa Burkina Faso karibu afunge bao dakika ya 17, lakini juhudi zake zikazimwa na kipa Yakoub Alo.
Feisal Abdallah karibu afungie Taifa Stars bao dakika ya 38 lakini naye alizimwa na mwamuzi aliyeamua kwamba aliotea.
Burkina Faso walirejea uwanjani kwa makeke wakiwa na malengo ya kutafuta bao la kusawazisha lakini hawakutumia vyema nafasi nyingi walizopata karibu na eneo la hatari.
Ulikuwa ushindi wa kihistoria kwa Tanzania ambayo ndio mara ya kwanza kuwahi kushinda mechi ya ufunguzi katika michuano ya CHAN, baada ya kushindwa mara mbili katika mashindano mawili yaliyopita.
Matokeo hayo yanaiweka Taifa Stars katika nafasi nzuri kwenye Kundi B ambalo pia linajumuisha Madagasgar, Mauritania na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Kwa upande wa Burkina Faso, safari ya kutafuta ushindi wa kwanza katika mechi za ufunguzi bado inaendelea.
Baada ya ushindi huo, Taifa Stars wanatarajiwa kuendeleza ubabe wao watakapokabiliana na Mauritania Jumatano, siku ambayo Burkina Faso watakutana na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Michuano ya mwaka huu inayoshirikisha timu 19 imeweka historia barani Afrika, kwani ni mara ya kwanza kuandaliwa na nchi tatu kwa wakati mmoja.
Lengo kuu la CAF kuanzisha CHAN mnamo 2009 ni kutoa nafasi kwa wachezaji wanaosakata soka kwenye ligi za nyumbani kuonyesha vipaji vyao machoni pa maskauti wa timu mbali mbali.
Ratiba ya mechi za leo
Niger vs Guinea (Mandela National Stadium),
Uganda vs Algeria (Mandela National Stadium).
Kesho (Agosti 5):
Senegal vs Nigeria (Amani Stadium, Zanzibar).