Dimba

Chapa Dimba All-Stars kuelekea Uhispania baada ya miezi minane ya subira

Na GEOFFREY ANENE September 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

TIMU  ya Safaricom Chapa Dimba All-Stars hatimaye imeratibiwa kuelekea nchini Uhispania hapo Septemba 6, 2025 kwa kambi ya mazoezi ya soka ya juma moja.

Jumla ya wachezaji 32 walichaguliwa kwenye mashindano ya Chapa Dimba yaliyoandaliwa na kampuni ya Safaricom kote nchini mwaka 2024. Vijana hao walifaa kusafiri Desemba 20, 2024, lakini hakuwezekana.

Ni wachezaji 25 sasa ndio watakuwa mjini Huesca kwenye kambi inayotarajiwa kuinua kiwango cha uchezaji wao.

Saba kutoka orodha ya kwanza tayari wamepiga hatua kwa kunyakuliwa na klabu za kitaifa na kimataifa. Safaricom inasema kuwa kunyakuliwa kwao ni ishara nzuri kuwa mashindano ya Chapa Dimba yanafanya kazi ya kutambua, kukuza na kufikisha talanta katika jukwaa la kimataifa.

“Lengo la Chapa Dimba ni kusaidia vijana kutoka Kenya kupata fursa na tunafurahia kuona ndoto zao zikitimia. Wachezaji kama Austin Odongo, Emily Moranga na Khamis Nyale wamejitosa katika soka ya malipo, wengine nao wamo mbioni kupitia kambi kama hii ya Uhispania. Hatua hizo zinatutia moyo kwa sababu Safaricom Chapa Dimba inalenga kuwapa vijana wetu nguvu, kubadilisha maisha yao na kuonyesha talanta ya Kenya katika ulingo wa kimataifa,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Safaricom PLC, Peter Ndegwa hapo Septemba 3, 2025.

Wakiwa Uhispania, vijana hao watazamia katika shughuli za kujiimarisha. Watapima ujuzi wao dhidi ya Akademia ya Huesca, kujifunza kutoka kwa wanasoka wa kulipwa na kutumia vifaa vya kisasa vya Base Aragonesa de Fútbol. Isitoshe, wachezaji pia watapata fursa ya kushuhudia mchuano wa Ligi ya Daraja la Pili kati ya SD Huesca na Malaga CF na kutalii mji huo.

Stanley Waswa kutoka akademia ya michezo ya Ndura Sports na Manda Sunira wa Highland Royals Moi Girls wataongoza timu ya Kenya. Wataandamana na makocha Chrispine Odindo kutoka Plateau Queens na Evans Oketch wa Obunga FC, na maafisa kutoka Shirikisho la Soka Kenya (FKF).