Deaf Harambee Stars, yaimarisha maandalizi kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (DAFCON
TIMU ya taifa ya soka ya wanaume ya wasio na uwezo wa kusikia ya Deaf Harambee Stars, imeimarisha maandalizi kuelekea mashindano ya kwanza ya Kombe la Mataifa ya Afrika (DAFCON), yatakayofanyika Addis Ababa, Ethiopia, kuanzia Novemba 30 hadi Desemba 13.
Baada ya kuteua kikosi cha wachezaji 25 mwezi Agosti, kikosi hicho kimekuwa kikipimana nguvu dhidi ya timu ambazo noi za wachezaji wa kawaida.
Kenya imepangwa Kundi D pamoja na Mali, Ghana na Zanzibar katika mashindano yatakayoshirikisha timu 17.
Oktoba 18, Deaf Harambee Stars iliifunga Boom Family FC mabao 3-1 katika Uwanja wa Riruta, Kawangware. Nahodha Philip Kirui alifunga mabao mawili huku Arafa Mohamed akipachika jingine.
Awali, kikosi hicho kinachonolewa na Kevin Njagi kilikuwa kimeilaza Ongata Rongai mabao 3-2 na Highway Secondary School 2-0.
Njagi, mwenye leseni ya ukocha ya CAF C, alisema maandalizi ya mapema yanalenga kuimarisha utimamu wa wachezaji, uwezo wa kiufundi na uelewa wa mbinu za mchezo.
“Tunalenga kujenga timu yenye nidhamu, ushindani na uimara wa kisaikolojia. Pia tunafanyia kazi mawasiliano uwanjani, frikiki, ulinzi, mashambulizi ya kushtukiza na kufunga,” alisema Njagi.
Alitambua kuwa kundi lao ni gumu, akitaja Mali kuwa mpinzani hatari zaidi kutokana na ushindi wake wa mabao 4-2 dhidi ya Kenya katika mashindano ya soka ya Afrika yaliyofanyika Uwanja wa Nyayo 2021.
Hata hivyo, alisema kikosi chake hakitishwi na wapinzani hao na kimejiandaa kupambana kwa ujasiri na nidhamu.
Changamoto zinazokikabili kikosi hicho ni pamoja na ukosefu wa viwanja vya mazoezi na mechi jijini Nairobi, pamoja na ukosefu wa fedha za kugharamia usafiri na mahitaji mengine.
Rais wa Shirikisho la Soka la Wachezaji wasio na uwezo wa kusikia Kenya (DFFK), Stephen Waweru, ameiomba sekta ya kampuni na wadau kujitokeza kufadhili timu wanapojiandaa kwa mashindano hayo.