Dimba

CAF yabadili msimamo, AFCON kila miaka miwili

Na TOTO AREGE November 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 1

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limebadili msimamo kuhusu ratiba ya kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), na kuamua kurejesha mfumo wa mashindano hayo kufanyika kila baada ya miaka miwili badala ya minne.

Hatua hiyo imekuja mwaka mmoja baada ya CAF kutangaza kuwa AFCON itaanza kuandaliwa kila baada ya miaka minne kuanzia 2028.

Ili kufidia pengo hilo, rais wa CAF, Patrice Motsepe, alikuwa ametangaza kuanzishwa kwa Ligi ya Mataifa ya Afrika (African Nations League), iliyopangwa kuanza 2029.

Hata hivyo, CAF ilifuta mpango huo baada ya kubaini kuwa ligi hiyo ingechukua muda mrefu kuanza kuzalisha mapato ya kutosha kugharamia mashindano yake.

Motsepe alisema kurejesha AFCON kila baada ya miaka miwili kunalenga kulinda maslahi ya soka ya Afrika, vyama 54 wanachama wa CAF na wachezaji wa bara hili wanaocheza katika klabu za nje.

Tangu 1968, AFCON imekuwa ikiandaliwa kila baada ya miaka miwili, isipokuwa 2012 na 2013 ambapo matoleo mawili yalifanyika kwa tofauti ya mwaka mmoja.

Toleo la 2025 nchini Morocco, lililofanyika kuanzia Desemba 21 hadi Januari 16, 2026, lilikuwa na mafanikio makubwa ya kibiashara. CAF ilisema mapato yake kutokana na mashindano hayo yaliongezeka kwa zaidi ya asilimia 90.

Idadi ya washirika wa kibiashara ilipanda kutoka tisa mwaka 2021 nchini Cameroon hadi 17 mwaka 2023 nchini Ivory Coast, kabla ya kufikia 23 la mwaka huu nchini Morocco.

Kwa mujibu wa Reuters, CAF ilipata faida ya dola 72 m (Sh9.3 b) kutokana na AFCON ya 2023, ikilinganishwa na dola 4m (Sh519.3 m) mwaka 2021.

AFCON ijayo itafanyika Juni 19 hadi Julai 17, 2027, Kenya, Uganda na Tanzania zikiwa wenyeji wa pamoja. Toleo linalofuata litafanyika 2028, kisha 2031 na 2033.

Awali, CAF ilipendekeza mfumo wa miaka minne ili kuoanisha mashindano hayo na kalenda ya kimataifa ya soka na kuepusha mgongano na msimu wa ligi za Ulaya.