Dogo apanga kurejea WAFCON kwa kishindo
MSHAMBULIAJI wa Harambee Starlets Mwanahalima Adam Jereko almaarufu “Dogo” amesema, amerejea Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 kwa mpigo.
Adam 28, alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kocha Beldine Odemba katika mechi za kufuzu dimba hilo la mwakani.
Alichangia mabao mawili dhidi ya Gambia katika mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya mwisho katika ushindi wa 3-1 na kufunga bao la pekee nchini Senegal katika ushindi wa 1-0 mechi ya marudiano.
Kenya ilishinda jumla ya mabao 4-1 dhidi na kujikatia tiketi ya kufuzu WAFCON kwa mara ya pili tangu 2016.
Adam alikuwa sehemu ya kikosi kilichofuzu kuwakilisha Kenya michuano ya WAFCON nchini Cameroon mwaka 2016, wakati Kenya ilifuzu kwa mara ya kwanza lakini hakusafiri na timu.
“Kurejea kwangu WAFCON mara hii ni spesheli kwangu kwa sababu, mwaka 2016 sikufanikiwa kusafiri na timu kutokana kwamba, nilikuwa najiaanda kufanya mtihani wa kidato cha nne,” alisema Adam mwanafunzi wa zamani wa Shule ya Upili ya wasichana ya St. Johns Kaloleni, Kilifi.
“Huu ndio wakati Wakenya kung’aa katika jukwaa kubwa Afrika,” aliongezea Adam mchezaji wa zamani wa Thika Queens na Hakkarigücü Spor ya Uturuki.
Mwaka wa 2016 Starlets walifuzu kwa mara ya kwanza chini ya kocha David Ouma baada ya kuibandua Algeria kwa jumla ya mabao 3-3 na kufuzu kutokana na faida ya mabao ya ugenini.
Starlets walipata sare ya 2-2 ugenini Adam akichangia bao na kutoka nyuma tena kulazimisha sara ya 1-1 jijini Nairobi.
Hivi sasa anaipigia klabu ya HB Koge ya Denmark kwa mkopo kutoka Kansas City Current ya Marekani. Anasema, kujiunga na Koge kwa mkopo kumechangia kuchezea Starlets.
“Niliko sasa napata nafasi ya kucheza ikilinganishwa na Marekani. Mimi sasa ni yule Dogo ambaye watu wanamfahamu. Wakati mwingine hatuangalii hela ama ukubwa au jina la klabu, ila nikutafuta nafasi ya kucheza,” alielezea Adam.
Kando na Adam, beki Enez Mango alicheza mechi za kufuzu WAFCON 2016 lakini hakusafiri na timu. Wacheza wa sasa wa Starlets beki Dorcas Shikobe, kiungo Corazone Aquino na mlinda lango Lilian Awuor waliocheza WAFCON nchini Cameroon ndio wachezaji pekee ambao wamesalia kikosini.
“Mara hii tunafaa kujipanga vilivyo. Tunataka kwenda kushindana na mataifa ambayo ya mabobea Afrika. Tunashukuru pia rais William Ruto ametukumbuka sisi kama mabinti na hii ni motisha kwetu,” aliongezea Adam.