Dimba

FA: Arsenal nyuma ya Man United dhidi ya Man City 

May 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

MASHABIKI wa klabu ya Arsenal wa kutoka ukanda wa Mlima Kenya sasa wamesema wanaunga mkono Manchester United ambayo itavaana na Manchester City katika fainali ya Kombe la FA ugani Wembley kuanzia saa kumi na moja jioni.

Katibu wa vuguvugu la Central4Arsenal Eliud Mwaura akiwa mjini Nyeri alisema kwamba haki na usawa ni kuunga mkono timu ya Man United “licha ya kuwa ni watani wetu wa tangu jadi”.

Alisema Jumamosi asubuhi kwamba busara hiyo ni kwamba, kwa kuwa timu za Arsenal, Man City, Liverpool, na Aston Villa zimejihakikishia kushiriki dimba la Klabu Bingwa Ulaya (Uefa), kuna haja ya timu ya Man United nayo iiingie kwa dimba la Europa.

“Baada ya timu ya Man United kukosa kutinga ndani ya mduara wa saba-bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kujipata nje ya mitanange ya Europa, njia pekee ya kurejea ni kuibuka bingwa wa FA msimu huu,” akasema Bw Mwaura.

Man United ikipata ushindi, basi itaingia moja kwa moja Europa.

Seneta Maalum Karen Nyamu licha ya kuwa shabiki sugu wa Arsenal, alisema kwamba wana fahari kuu kwa kumaliza msimu wa EPL wakiwa wa pili nyuma ya Man City na pia juu ya Man United.

Kwa hili la FA, Bi Nyamu alisema hana la kufia.

“Lakini ninawatia shime hawa watani wetu wa Man United wajikakamue angalau waangukie mfupa na makombo ya Ulaya,” akasema Bi Nyamu.

Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ambaye ni shabiki wa Man United alisema kwamba kwa sasa hajui mjadala ni wa nini.

“Sisi hupata ushindi tukipenda na hata ikitokea tumepoteza mechi, huwa ni kutaka kwetu,” akasema Bw Nyoro.

Naye Bw Mwaura alidai kwamba mashabiki wa Liverpool na Chelsea wameungana kuombea Man United kilio cha FA guuni mwa Man City lakini “sisi wanaArsenal daima hatutawahi kujihusisha na ukatili wa kumponda vibonde aliye chini”.

Alisema kwamba Man United kwa sasa ni sawa na jamii ya wasiobahatika.

“Sisi mashabiki wa Arsenal ni watu wa maombi, haki na usawa tunaMuomba Mungu wetu awajalie Man United ushindi ndio hata nao wawe na la kupigia mdomo wakijiandaa kushiriki dimba la Europa,” akasema.