FA: Opta inasema Arsenal kichwa dhidi ya Man U, lakini historia yaonyesha yeyote anaweza
NANI ataenda nyumbani mapema kati ya Arsenal na mabingwa watetezi Manchester United kwenye Kombe la FA la 2024-2025?
Mbivu na mbichi kuhusu mafahali hao wawili itajulikana Jumapili saa kumi na mbili jioni wakati wanabunduki wa Arsenal wataalika mashetani wekundu wa United katika mechi za raundi ya tatu.
Timu zote kutoka Ligi Kuu huanza kipute hicho katika raundi ya tatu inayojumuisha timu 64. Droo ilipofanywa, Arsenal na United na pia Aston Villa na West Ham ndizo pekee kutoka Ligi Kuu zilikutanishwa. Timu nyingine za Ligi Kuu zilipata washiriki kutoka ligi za chini katika raundi hii.
Kompyuta ya Opta inapatia Arsenal asilimia 71.4 ya kutwanga Manchester United ndani ya dakika 90.
Ni mara ya kwanza kabisa Arsenal na United watavaana katika raundi ya tatu ya Kombe la FA.
Licha ya kuwa Arsenal inakamata nafasi ya pili ligi nayo United ni ya 13, historia kati ya timu hizo kwenye Kombe la FA inaonyesha kuwa mchuano huu unaweza kuenda popote.
Takwimu zinaonyesha kuwa Arsenal wamebandua mabingwa watetezi wa Kombe la FA mara sita mfululizo wamekutana, wakifanya hivyo mara ya mwisho kwa kucharaza Manchester City 2-0 katika nusu-fainali msimu 2019-2020. Hata hivyo, United wamezidia Arsenal maarifa mara tatu kati nne zilizopita kwenye kipute hicho ikiwemo 3-1 mara ya mwisho walionana ugani Emirates mnamo Januari 2019.
Hakuna pia timu nyingine imeumiza Arsenal mara nyingi katika Kombe la FA kama United (nane) nayo Arsenal pia ni timu imetupa United nje ya kipute hicho mara nyingi (saba).
Katika misimu miwili kati ya tatu iliyopita, Arsenal waliaga mashindano hayo katika raundi ya tatu kwa hivyo watalazimika kuwa makini na katili zaidi wasipate masaibu zaidi.
Makocha Mikel Arteta (Arsenal) na Ruben Amorim (United) wanatarajiwa kufanya maamuzi makubwa kuhusu wachezaji watakaowatumia.
Amorim amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Uingereza akisema atachezesha kikosi chake kikali kabisa, ingawa atampa fursa Altay Bayandir kujaza nafasi ya kipa nambari moja Andre Onana.
Arteta naye atalazimika kujikuna zaidi kichwa kuhusu wachezaji atatwika majukumu ya kibarua hicho kwa sababu mpepetano mwingine mkali wa Ligi Kuu dhidi ya Tottenham unanukia hapo Januari 14.
Arsenal wanaomezea mate mshambulizi wa United, Marcus Rashford, watategemea Gabriel Martinelli kutafuta mabao naye nahodha Bruno Fernandes ataongoza shughuli ya mashetani wekundu.
Arsenal na United ndizo timu zimeshinda Kombe la FA mara nyingi. Wanabunduki wa Arsenal wana mataji 14 nao United 13.
Timu hizo zitajibwaga uwanjani baada ya kusajili matokeo mseto katika mechi zilizopita. Arsenal walikula 2-0 kutoka kwa Newcastle katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Carabao Cup mnamo Januari 7 nao United wakapata motisha ya sare ya 2-2 ligini dhidi ya viongozi wa ligi Liverpool hapo Januari 5.