Fabregas mbioni kuwa kocha mpya wa Leverkusen iliyompiga teke Ten Hag
LEVERKUSEN, Ujerumani
CESC Fabregas anapigiwa upatu kuwa kocha mpya wa Bayer Levekusen ambayo imepiga kalamu kocha wa zamani wa Manchester United Erik ten Hag mnamo Jumatatu, Septemba 1, 2025.
Nyota huyo wa zamani wa Uhispania na klabu ya Arsenal ni kocha wa Como kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A).
Aliongoza Como kupandishwa ngazi 2023-2024 na kusalia juu baada ya kukamilisha msimu 2024-2025 katika nafasi ya 10 kutoka orodha ya klabu 20.
Leverkusen inashiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga). Imetema Ten Hag kutoka Uholanzi baada ya michuano miwili tu ya Bundesliga ambayo ilipoteza 2-1 mikononi mwa Hoffenheim hapo Agosti 23 kabla ya kutupa uongozi wa mabao 3-1 ikitoka 3-3 na Werder Bremen mnamo Agosti 30.
Fabregas,38, ambaye ni mmoja wa wamiliki wa Como, alianza kazi ya ukocha katika klabu hiyo ka kutia makali timu ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 19 msimu 2023-2024 na kupanda kwa haraka kabla ya kuwa kocha mkuu mnamo Julai 19, 2024.
Kandarasi yake na Como kama kocha mkuu inafaa kutamatika Juni 30, 2028.
Hata hivyo, kazi yake ya kuridhisha imevutia mabingwa wa Bundesliga 2023-2024 Leverkusen.
Fabregas, ambaye amehitimu kama kocha na leseni ya soka ya malipo ya Shirikisho la Soka barani Ulaya (Uefa), amedokeza mara kadhaa kuwa yuko tayari kuhama Como.
Ripoti sasa zinadai kuwa Fabregas ameanza kufanya mazungumzo na Leverkusen. Makocha wasaidizi Rogier Meijer na Andries Ulderink wametwikwa majukumu ya kuongoza klabu hiyo inapoendelea kutafuta kocha mpya ikiwemo kuzungumza na Fabregas.