Dimba

FKF Kiambu yazindua tuzo za ligi ya kaunti

Na TOTO AREGE November 3rd, 2026 Kusoma ni dakika: 2

TAWI la Shirikisho la Soka nchini (FKF) katika kaunti ya Kiambu, limeanzisha utaratibu wa kutambua na kutuza wachezaji waliofanya vizuri katika ligi za kaunti hiyo msimu jana.

Hii ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuinua viwango vya soka mashinani, kuimarisha ushirikiano kati ya wadau na kutoa nafasi zaidi kwa vijana kukuza vipaji vyao.

Tawi hilo linalenga kuendeleza utamaduni wa kutambua ubora, kuhamasisha vipaji na kutumia soka kama nyenzo ya kubadilisha maisha ya vijana.

Hayo yalijiri wakati tawi hilo lilipoandaa kwa mara ya kwanza hafla ya utoaji tuzo kwa wachezaji na waamuzi waliofanya vizuri katika ligi za kaunti hiyo msimu wa 2025/2026.

Hafla hiyo ilifanyika katika Ijumaa ukumbi wa Havilah Cornerstone Ranch, Ruaka, na kuwakutanisha wadau wa soka, wachezaji, makocha, maafisa wa timu pamoja na wageni waalikwa.

Wachezaji waliofanya vizuri katika ligi za wanaume na wanawake walituzwa katika vipengele mbalimbali, vikiwemo mchezaji bora wa msimu, kocha bora, mfungaji bora na kipa bora.

Miongoni mwa waliotuzwa ni Stephen Ng’ang’a wa Miiri FC, aliyetwaa tuzo ya mfungaji bora na alisema;

“Msimu ulikuwa na changamoto nyingi, lakini nisingeweza kufanikiwa bila timu nzima na Mungu ambaye alinijalia. Ujumbe wangu ni mmoja tu kwa vijana ambao wamekata tamaa wakiwa nyumbani, msife moyo hata kama kipaji chenu hakijawalipa kwa sasa. Tuzidi kupambana tu.”

Kwa upande wake, mdhamini wa hafla hiyo, Lennah Koinange, aliwataka vijana kutumia fursa walizonazo kucheza soka na kufurahia safari yao ya kimichezo.

“Huu ndio wakati wenu wa kucheza. Furahieni wakati huu kwa sababu huu ndio wakati mlio nao.”

Timu ya St Andrewes ya wanaume ilipokea Sh 200,000 kwa kuchukua ubingwa wa ligi sawa na Unity Homes Ladies FC ya mabinti ambao walienda nyumbani na Sh 100,000 kwa kuwa mabingwa.

Aidha, aliyekuwa kiungo wa zamani wa Harambee Stars, Francis Kahata, alitambuliwa kwa mchango wake mkubwa katika soka kupitia tuzo ya kutambua mchango wake wa maisha yote katika mchezo huo.

Tuzo hiyo ilitambua mafanikio yake katika taaluma ya soka pamoja na mchango wake katika kuhamasisha kizazi kipya cha wanasoka.

Hafla hiyo iliwezeshwa na Serikali ya Kaunti ya Kiambu pamoja na Koinange, ambao wamechangia katika maendeleo ya michezo na uwezeshaji wa vijana.

FKF Kiambu imesema itaendeleza juhudi hizo katika misimu ijayo kwa lengo la kujenga msingi imara wa soka mashinani na kuhakikisha vipaji vinapata jukwaa la kuonyesha uwezo wao.