Furaha mwanadada mwanasoka nguli wa Zetech akipata ufadhili wa kusomea Amerika
MWANADADA matata wa soka wa Chuo cha Zetech, Ruiru kaunti ya Kiambu, Rebecca Kwoba, amepata ufadhili wa masomo katika chuo cha Alcorn State nchini Amerika.
Mrembo huyo alifanya somo la uhandisi huku pia akipiga soka.
Kwoba aliwakilisha timu ya Kenya Harambee Starlets katika mashindano ya kombe la Dunia mwaka wa 2023 alipokuwa nahodha wa kikosi hicho.
Mwanadada huyo alihudumu katika kiungo na difensi huku akionyesha ubora wake katika soka.
Wakati huo pia, Kwoba aliwakilisha kikosi cha Rising Starlets mwaka wa 2024 kwa mashindano ya wanawake FIFA, ya kikosi cha wachezaji wasiozidi miaka 20.
Mwanadada huyo alipongeza chuo cha Zetech kwa kumlea hadi akapiga hatua hiyo.
Kocha mkuu wa Zetech Sparks FC Herriet Fakhir, alipongeza Kwoba, kwa juhudi zake za kuinua kikosi cha Zetech na kuliweka katika ramani ya ulimwengu.
Alisema kiungo huyo matata alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Zetech waliodumisha ñidhamu ya hali ya juu.
Naibu Chansela wa Chuo cha Zetech Prof Njenga Munene, alipongeza mrembo huyo kwa kujizatiti vilivyo darasani na viwanjani.
Alisema chuo hicho inatilia mkazo zaidi maswala ya masomo na michezo kwa sababu zimeonyesha mafanikio katika maisha.
Wakati huo pia mwanafunzi wa Zetech aliyeonyesha ubora wake katika vikapu Madina Okot, mwezi Disemba, 2024 alipata ufadhili kupata elimu katika chuo cha Mississippi, Amerika.
Alisema kwa wakati huu chuo cha Zetech inatilia mkazo wanafunzi kuzamia katika michezo ya soka, vikapu, na hata riadha, ili waweze kupata mwanya wa kusafiri ng’ambo kutokana na vipaji vyao.