Dimba

Gor, Police, Tusker ulingoni tena vita vya kuwania ubingwa KPL vikichacha wikendi

Na CECIL ODONGO May 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kudondosha alama katikati mwa wiki, Kenya Police, Tusker na Gor Mahia zinarejea ulingoni tena mechi za Ligi Kuu (KPL) zikiingia raundi ya 32.

Baada ya mechi za wikendi hii, zitakuwa zimesalia michuano miwili pekee msimu huu utamatike. Kenya Police inaongoza kwa alama 58, Tusker (55), Gor (53), Shabana (52) na Kakamega Homeboyz (51).

Timu hizo zote zimecheza mechi 31 isipokuwa Gor ambayo ina mchuano moja kibindoni baada ya Debi ya Mashemeji iliyostahili kusakatwa wikendi iliyopita kuahirishwa.

Katikati mwa wiki, Kenya Police walipigwa 2-1 na Kakamega Homeboyz, Tusker ikapoteza 2-0 dhidi ya FC Talanta nayo Gor ikachapwa 2-1 na Nairobi City Stars inayopambana kusalia KPL.

Kenya Police itavaana na FC Talanta Jumapili katika uga wa Kenyatta, Kaunti ya Machakos huku Gor ikisafiri siku hiyo hiyo kupambana na Murang’a Seal uwanja wa Sportpesa Arena, Murang’a.

Tusker nao watakuwa jijini Nairobi uga wa Dandora kuvaana na Sofapaka. Shabana watakuwa wenyeji wa Mara Sugar ugani Gusii nao Homeboyz wavaane na Kariobangi Sharks uwanja wa Dandora, mechi zote zikisakatwa Jumapili.

Hata hivyo, macho yote yatakuwa kwa timu tatu za juu ambazo zinalenga ubingwa wa KPL na zimekuwa zikionyesha matokeo ya kuridhisha.

Kenya Police wana kibarua kikubwa ikizingatiwa FC Talanta si mpinzani rahisi kwa kuwa imepiga Gor, Tusker, AFC Leopards na Sofapaka.

Je Kenya Police watatoboa ama juhudi zao za kusaka ubingwa zitapata pigo tena?

Police wameshindwa mara moja pekee na  FC Talanta ambao walipanda nao KPL mnamo 2022.  Timu hizo zimecheza mechi saba, Kenya Police wakishinda mara mbili huku nyingine nne zikiishia sare.

Pia mbio za kutwaa Kiatu cha Dhahabu zitaendelea kuwa ngumu Moses Shumah wa Kakamega Homeboyz na Emmanuel Osoro wa FC Talanta wakiongoza wakiwa wamefunga mabao 16 kila moja.

Kwa upande mwingine, timu ambazo zitashushwa ngazi bado ni vigumu kujilikana ikizingatiwa nambari 10 na 18 zimetenganishwa na alama nane.

Ratiba ya KPL

Jumamosi

Sofapaka v Tusker (Dandora, Nairobi, 1pm)

Mathare United v Ulinzi Stars (Dandora, Nairobi, 4pm)

JUMAPILI

Murang’a Seal v Gor Mahia (Sportpesa Arena, Murang’a, 3pm)

Bandari v AFC Leopards (Mbaraki, Mombasa, 3pm)

Kariobangi Sharks v Kakamega Homeboyz (Dandora, Nairobi, 4pm)

Nairobi City Stars v Posta Rangers (Kenyatta, Machakos, 1pm)

Kenya Police v FC Talanta (Kenyatta, Machakos, 4pm)

Shabana v Mara Sugar (Gusii, Kisii, 2pm)

Jumatatu

Bidco United v KCB (Kenyatta, Machakos, 3pm)