Dimba

Guardiola arejea Uhispania kisiri kujaribu kuokoa ndoa yake na Cristina

Na CHRIS ADUNGO March 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IMEFICHUKA kuwa kocha Pep Guardiola alifunga safari ya siri ya siku tatu kwenda Barcelona kujaribu kuokoa ndoa yake kwa kukaa pamoja na mkewe Cristina nyumbani kwao Uhispania.

Inaonekana kuwa mkufunzi huyo wa Manchester City “hajakata tamaa kuhusiana na ndoa yake” licha ya tangazo la talaka mnamo Januari 2025, vyanzo vya habari vinasema.

Guardiola, 54, aliabiri ndege ya kibinafsi kutoka jijini Manchester hadi Barcelona saa chache baada ya timu yake kushinda Plymouth Argyle 3-1 kwenye raundi ya tano ya Kombe la FA ugani Etihad mwanzoni mwa mwezi huu.

Man-City walikuwa na siku saba za kupumzika kabla ya kupokezwa kichapo kichungu cha 1-0 na Nottingham Forest katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) uwanjani City Ground wikendi iliyopita.

Chanzo kimoja kilisema: “Guardiola na Cristina walikaa pamoja kwa siku tatu huko Barcelona, wote wakiishi pamoja katika kasri lao la familia. Kocha huyo aliondoka nyumbani Jumatatu asubuhi ya Machi 3, 2025 kwenda kuona daktari wa meno naye Cristina akaenda kwa shughuli za biashara katika duka lake la bidhaa za uanamitindo katikati mwa jiji la Barcelona.”

“Walikutana tena dukani baadaye jioni na kukaa hapo kwa saa tatu kabla ya kurudi nyumbani. Ingawa haijulikani iwapo walilala pamoja katika chumba kimoja na kitanda kimoja, ukweli ni kwamba walilala katika nyumba yao wanayoimiliki viungani mwa jiji la Barcelona. Guardiola aliondoka katika kasri hilo asubuhi ya siku iliyofuata.”

Safari hiyo imezua matumaini kwamba wawili hao huenda wakawasha upya mwenge wa penzi lao na kurudiana kwa lengo la kuokoa ndoa yao.

Japo walitengana rasmi mnamo Januari mwaka huu, ndoa yao ilianza kuingia mdudu mnamo 2019 baada ya Cristina, 52, kuondoka jijini Manchester na kurejea Barcelona.

Ndoa ya Cristina na Guardiola imejaliwa watoto watatu – Valentina, 17, Marius, 22, anayeishi Dubai na Maria, 24, ambaye anaishi London.

Kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich ambaye ameapa kutovua pete yake ya ndoa, atakuwa amekamilisha miaka 11 ugani Etihad mkataba wake mpya kambini mwa Man-City utakapomalizika rasmi Novemba 2026. Tayari ndiye mkufunzi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi katika EPL kwa sasa.