Dimba

Hapa kwa Real Madrid na Man City anakufa mtu!

February 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MADRID, UHISPANIA

LEO mechi nne za Klabu Bingwa barani Ulaya zitasakatwa, huku mashabiki wengi wakitarajiwa kuelekeza macho yao katika pambano kati ya wenyeji Real Madrid na Manchester City ugani Santiago Bernabeu.

Ni mechi ambayo kocha Pep Guardiola anaamini kikosi chake kina nafasi ndogo zaidi ya kushinda baada ya kuchapwa 3-2 katika mkondo wa kwanza.

Hata hivyo, vigogo hao wataingia uwanjani na matumaini makubwa baada ya kuandikisha ushindi mkubwa wa 4-0 dhidi ya Newcastle United kwenye pambano la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mwishoni mwa wiki.

Kwa upande mwingine, Madrid walikuwa na kazi ngumu baada ya kupoteza pointi mbili kutokana na sare ya 1-1 dhidi ya Osasuna, matokeo ambayo yameiwezesha Barcelona kuwapiku kwenye msimamo wa La Liga.

Wengi wanatarajia wenyeji kuibuka na ushindi kutokana na rekodi nzuri ya Carlo Ancelotti dhidi ya Guardiola katika hatua ya muondoano baada ya awali kuwabandua katika msimu ya 2013-14, 2021-2022 na 2023-24.

Jijini Dortmund, wenyeji Borussia Dortmund wataalika Sporting Lisbon ugani Westfalen huku wakijivunia ushindi wa 3-0 wa mkondo wa kwanza ambapo Serhou Guirassy alifunga bao lake la 10 siku hiyo.

Baada ya ushindi huo, hatimaye wenyeji walishindwa kuendeleza ubabe wao kwenye Ligi Kuu ya Bundesliga waliposhindwa 2-0 na Bochum, Jumamosi.

Mechi ya leo imejiri wakati kiwango cha Sporting kimeshuka, baada ya kushinda mechi moja tu kati ya tano katika mashindano mbalimbali.

Baada ya kushindwa katika mkondo wa kwanza, kikosi hicho cha kocha Joao Fereira kilitoka sare ya 2-2 na Arouca nyumbani kwenye mechi ya Primeira Liga, Jumamosi.

Viktor Gyokeres hakufunga kwenye pambano hilo, lakini alimwandalia pasi Conrad Harder aliyefunga bao la katika kipindi cha kwanza.

Dortmund almaarufu Die Schewarzgelben wameshinda mechi mbili katika mechi nne mwezi huu, ingawa ushindi huo ulitokea kwenye mechi za ugenini.

Wenyeji wanajivunia rekodi nzuri ya asilimia 100 dhidi ya timu za Ureno, rekodi ambayo inawapa matumaini makubwa ya kushinda.

Elix Nmecha ataendelea kubakia nje kutokana na jeraha, huku Carney Chukwuemeka aliyekosa kucheza dhidi ya Bochum akitarajiwa kuwa kikosini baada ya kurejea mazoezini siku chache zilizopita.

Kadhalika, Ramy Bensebaini anatatizwa na jeraha na huenda akakosa kuanza kikosini.

Kwa upande mwingine, kocha Niko Kovac atakuwa bila Geny Catamo, Nuno Santos na Pedro Goncalves wanaoguuza majeraha, pamoja na Daniel Braganca aliyeumia kwenye mechi iliyopita dhidi ya Arouca.

Vile vile Jeremiah St Juste aliumia katika mechi hiyo, huku hali yake ikiendelea kuchunguzwa na madaktari wa klabu hiyo.

Kwingineko, limbukeni Brest ya Ufaransa itakuwa ugenini kucheza na Paris Saints-Germain (PSG) huku PSV ya Uholanzi ikikaribisha Juventus ya Italia jijni Endhoven.

Ratiba ya Jumatano:

Borussia Dormund vs Sporting Lisbon (8:45pm), Real Madrid vs Manchester City (11pm), PSG vs Brest (11pm), PSV vs Juventus (11pm).