Hawa Nottingham watapatia Liverpool kipigo kingine walivyofanya msimu ukianza?
NOTTINGHAM Forest watakuwa wenyeji wa vinara wa ligi Liverpool katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani The City Ground, Jumanne kuanzia saa mbili usiku.
Liverpool ambao wana mechi moja kiporo, wanaongoza jedwali na alama 46 baada ya mechi 19.
Nottingham nao ni miongoni mwa timu ambazo zimeng’aa msimu huu na wameshikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi na alama 40 sawa na Arsenal nafasi ya pili.
Kufuatia ushindi wa 1-0 ugani Anfield katika mkondo wa kwanza mwezi Septemba, Nottingham wanatazamia kupata alama zote sita kutoka kwa Liverpool msimu huu kwa mara ya pili tangu msimu wa 1962-63.
Nottingham wameshinda kila mechi kati ya mechi sita zilizopita za EPL, na ushindi dhidi ya Liverpool utawafanya kuwa sawa na msururu wao mrefu zaidi wa kushinda ligi kati ya saba, iliyowekwa mara nne awali (Februari 1893, Desemba 1906, Oktoba 1921, na Septemba 1979).
Mechi zingine tatu zimepangwa Jumanne na katika mechi nyingine ya kukata na shoka, Brentford wako tayari kuendeleza rekodi yao ya kujivunia nyumbani watakapowakaribisha mabingwa wa watetezi Manchester City.
Wenyeji wamepoteza mechi mbili mtawalia wakiwa nyumbani chini ya kocha Thomas Frank na wana pointi 22 katika uwanja wa Gtech Community, huku Liverpool pekee ikijivunia rekodi bora nyumbani (23).
Mara ya mwisho walicheza nyumbani, Brentford iliichapa Southampton 5-0, matokeo ambayo Frank anaamini ni miongoni mwa matokeo ya kuvutia msimu huu.
Hata hivyo, walishtushwa na Plymouth katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA Jumamosi, wakichapwa 1-0.
City, wakati huo huo, waliilaza Salford 8-0 na kutinga raundi ya nne, huku James McAtee akifunga hat-trick naye Jack Grealish akifunga bao kwa mara ya kwanza tangu Desemba 2023.
Chelsea nao watakuwa nyumbani Stamford Bridge kumenyana na Bournemouth huku West Ham ikiialika Fulham ugani London Stadium.
Ratiba ya mechi za Jumanne
Brentford vs Manchester City (7:30 pm)
Chelsea vs Bournemouth (7:30 pm)
West Ham vs Fulham (7:30 pm)
Nottingham Forest vs Liverpool (8:00 pm)