Dimba

Hela ndefu Liverpool imemwaga sokoni licha ya kushinda EPL zashtua mahasimu

Na GEOFFREY ANENE July 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LIVERPOOL, Uingereza

Liverpool imefikisha Sh43.6 bilioni ambazo imemwaga sokoni kujisuka baada ya kusajili wa mshambulizi Hugo Ekitike kutoka Eintracht Frankfurt kwa Sh12 bilioni (Pauni 69 milioni).

Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 23 amefanyiwa vipimo vya afya na pia amekubaliana masharti binafsi, na atajiunga na kikosi cha Reds katika ziara ya maandalizi ya msimu mpya barani Asia wiki hii.

Mkataba huo kwa jumla unafikia hadi Sh13.8 bilioni, ukiwemo ongezeko la Sh1.7 bilioni kulingana na mchango wake katika mafanikio ya Liverpool.

Usajili wake umefikisha matumizi ya fedha ya Liverpool katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho kuwa zaidi ya Sh43.6 bilioni baada ya kununua Florian Wirtz kwa Sh20.2 bilioni na mabeki Milos Kerkez na Jeremie Frimpong kwa jumla ya Sh12.2 bilioni.

Ofa ya Newcastle ya Sh12.2 bilioni kwa Ekitike mapema mwezi huu ilikataliwa.

Ekitike alikuwa na msimu mzuri katika Ligi Kuu ya Ujerumani, akifunga mabao 15 na kuchangia asisti nane katika mechi 31 alizoanza.

Pia, Ekitike aliongoza ligi kwa jumla ya makombora yaliyolenga lango (117), akiisaidia Frankfurt kumaliza katika nafasi ya tatu.

Wakati huo huo, Ipswich Town imeajiri beki mkongwe Ashley Young kwa kandarasi ya mwaka mmoja.

Young, 40, aliondoka Everton mwishoni mwa msimu uliopita.

Ameshacheza michuano 750 za klabu na ana mataji 39 na timu ya taifa ya Uingereza.

“Ashley amekuwa na taaluma bora,” alisema kocha wa Ipswich Kieran McKenna.

“Uongozi na taaluma yake vitakuwa na umuhimu mkubwa msimu huu.”

Ipswich watafungua msimu Ligi ya Daraja la Pili dhidi ya Birmingham City mnamo Agosti 8.

Nchini Uhispania ni kuwa Marcus Rashford amejiunga na Barcelona kwa mkopo wa msimu mzima kutoka Manchester United.

Rashford, 27, anakuwa Muingereza wa kwanza kusaini kwa klabu hiyo tangu Gary Lineker mwaka 1986.

Barca wana chaguo la kumsajili kabisa mwaka 2026 kwa Sh5.2 bilioni (Pauni 30.3 milioni).

Rashford, ambaye hajachezea United tangu Desemba baada ya kutofautiana na kocha Ruben Amorin, alicheza nusu ya pili ya msimu 2024-2025 kwa mkopo Aston Villa.

Sasa, anajiunga na mabingwa wa La Liga na Copa del Rey, akisema, “Ninajihisi kama niko nyumbani.”