Jinsi Harambee Stars walikata kucha za ‘Chui’ wa DR Congo pale Kasarani
KOCHA wa Harambee Stars Benjamin McCarthy alitumia ufundi mkubwa kuhakikisha kuwa Kenya inatamba dhidi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kuwahi ushindi wake wa kwanza kwenye Kombe la Afrika kwa Wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024).
Kenya Jumapili iliwahi ushindi kwenye mechi hiyo ya Kundi A iliyogaragazwa uga wa Kasarani kupitia bao la kiungo wa Gor Mahia Austin Odhiambo dakika ya tatu zilizoongezwa baada ya zile dakika 45 za kwanza kukamilika.
Odhiambo aliuwahi mpira huo kutoka kwa Masud Juma baada ya Daniel Sakari kuwalemea wachezaji wa DR Congo upande wa kulia na kufunga mpira ambao ulimlemea kipa Brudel Efonge.
McCarthy alipanga kikosi ambacho kilikuwa na kasi ila mara si moja, safu ya kati ilionekana kulemewa na wanasoka wa DR Congo.
Odhiambo na Kiungo mwenzake wa Gor Alpha Onyango walionekana kuwa na wakati mgumu kuhimili kasi ya wachezaji wa Leopards ya DRC.
Kwa upande mwingine, Masoud Juma naye alijaribu krosi za mbali ila mvamizi Ryan Ogam hakuwa akiziwahi kwa wakati mara nyingi mabeki wa DR Congo wakiuondoa mpira.
Kulemewa huku ndiko kulifanya Kenya ifungwe dakika ya tano baada ya mechi kuanza pale nahodha Aboud Omar alipoteza mpira nje ya kijisanduku na Jephte Kitamba akafungia DR Congo.
Kenya ilipata nafuu baada ya refa kuangalia VAR na kulifuta bao lenyewe kwa sababu Daniel Sakari alikuwa amekanyagwa kuelekea kufungwa kwa goli hilo.
Kenya iliingia mchezoni kihalisi baada ya nusu saa na ikatekeleza mashambulizi makali huku mipira ikiangukia Masud Juma na David Sakwa.
Kabla ya Kenya kufunga, Ogam alikuwa amemegewa pasi safi na Sakwa lakini mshambulizi huyo wa Tusker akaachilia fataki mbovu.
Kipindi cha pili DR Congo walimiliki sana mpira lakini mabadiliko aliyofanya McCarthy yalihakikisha Kenya inalinda uongozi wake.
Marvin Nabwire na Boniface Muchiri walioingia nafasi ya Manzur Okwaro na Juma, walifanya kazi kubwa kudhibiti mpira na kuhakikisha Stars inashinda mchuano huo.
Zikiwa zimesalia dakika saba mechi ikamilike, Kenya ilikuwa nafasi ya kuongeza bao la pili na kumaliza mchezo au kuzamisha DR Congo kabisa lakini haikufanikiwa.
Odhiambo alimmegea Ben Stanley mpira baada ya kuingia nyuma ya mabeki wa DR Congo. Akiwa na kipa wa DR Congo pekee kumpita, Stanley aliupiga mpira wa juu ambao ulienda nje wakati mashabiki walikuwa washasimama.
Baada ya kuwahi ushindi huo, Kenya sasa inahitaji kuchukua alama tatu dhidi ya Angola mnamo Jumatano kufuzu hatua ya robo fainali.
“Tumecheza vizuri na hata wakati ambapo presha zilikuwa zimezidi, vijana walidhibiti mchezo na kupunguza kasi ya wanasoka wa DR Congo,” akasema McCarthy.
“Hakuna nafasi ya kusherehekea bali tunastahili kujipanga na kuvumbua mbinu za kupiga Angola. Kile kilichonifurahisha ni kwamba tulicheza mpira wa kuvamia japo kipindi cha pili tulilemewa lakini bado tukadhibiti mchezo,” akaongeza.
Mwenzake wa DR Congo Otis Ngoma alikiri kwamba vijana wake walikosa kubuni nafasi za kufunga na kupenya ngome ya Kenya.
“Sasa lazima tuamke na tushinde mechi yetu ijayo dhidi ya Morocco. Tulishindwa kabisa kupenya safu ya nyuma ya Kenya na pia nafasi tulizozipata hatukuzitumia vizuri,” akasema.
Mechi hiyo ilihudhuriwa na Rais William Ruto, Kinara wa Upinzani Raila Odinga na halaiki ya mashabiki wa soka ambao walishangilia na kusherehekea bao la vijana wa nyumbani.
Ushindi huo sasa unahakikishia kila mchezaji wa Stars tunu ya Sh1 milioni ambazo aliahidi Rais William Ruto alipotembelea kambi ya timu hiyo mnamo Jumamosi.