Dimba

Jumanne ya drama tele kwa Chelsea, Tottenham na Liverpool UEFA

Na REUTERS December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BERGAMO, ITALIA

CHELSEA, Tottenham na Liverpool walishuhudia usiku wenye drama kubwa kwenye Klabu Bingwa Ulaya hapo Jumanne, usiku ambao bahati ilibadilika ghafla kwa vigogo hao watatu wa Uingereza.

Chelsea walipata pigo kubwa mikononi mwa Atalanta nchini Italia, Tottenham wakazoa ushindi mnono nyumbani jijini London, huku Liverpool wakipata ushindi wa dakika za mwisho wenye utata dhidi ya Inter Milan ugani San Siro.

Matokeo hayo yalikuwa na uzito wake, yakichangia kuunda taswira pana ya hatua ya ligi kadri ushindani unavyozidi kuwa mkali.

Matumaini ya Chelsea ya kufuzu moja kwa moja kwa hatua ya muondoano ya ligi hiyo ya klabu 36 yalipigwa chini vibaya baada ya Atalanta kuwafunga 2-1 mjini Bergamo.

Timu zote mbili ziliingia uwanjani zikiwa na ushindi tatu, sare moja na kipigo kimoja na hivyo kuwa na pointi 10 kila moja.

Kwa kipindi kikubwa cha mchezo kulikuwa na uwiano mkubwa, na Chelsea hata walitangulia kipindi cha kwanza kupitia Joao Pedro aliyemalizia krosi nzuri ya Reece James.

Hata hivyo, Atalanta waliendelea kuwa tishio walipofanya mashambulizi, winga wa zamani wa Charlton na Everton Ademola Lookman akiwahangaisha mabeki wa Chelsea.

James alipiga mpira fyongo baada ya mapumziko, lakini wenyeji waliweka presha zaidi na hatimaye kusawazisha 1-1 kupitia kichwa safi mvamizi wa zamani wa West Ham, Gianluca Scamacca.

Baada ya hapo, Alejandro Garnacho alimjaribu kipa wa Atalanta, lakini baadaye safu ya ulinzi ya Chelsea ikatikiswa na Charles de Ketelaere aliyefumua kombora moto hadi nyavuni dakika za lala-salama.

Pedro alinyimwa bao la kusawazisha na kipa Marco Carnesecchi.

Chelsea wameshuka kutoka nafasi za juu nane hadi ya 11, huku michezo miwili tu ikibaki.

Kipigo hicho kiliendeleza matokeo ya kusikitisha ya Chelsea, ambao sasa hawajapata ushindi katika mechi nne tangu wabomoe Barcelona 3-0 mwishoni mwa Novemba.

Kocha Enzo Maresca alifanya mabadiliko matano usiku Jumanne, akiendeleza mtindo alioonyesha majuzi.

Alijitetea, akisema wachezaji tegemeo bado ni wale wale, na akawakumbusha wakosoaji kwamba wachezaji wanane ama tisa wa kikosi cha kwanza walicheza dhidi ya Tottenham, Barcelona na Arsenal.

Kwingineko, Liverpool waliduwaza wenyeji Inter Milan 1-0 ugani San Siro kupitia penalti ya utata dakika za mwisho.

Dominik Szoboszlai alifunga penalti hiyo baada ya Florian Wirtz kuanguka ndani ya kisanduku kwa urahisi kufuatia kuvutwa shati na Alessandro Bastoni.

Kocha Arne Slot alisifu uthabiti wa kikosi chake.

Wakati huohuo, Tottenham walikuwa na kazi rahisi zaidi, wakibamiza Slavia Prague 3-0 kupitia bao la kujifunga la David Zima na penalti zilizojazwa kimiani na Mohammed Kudus pamoja na Xavi Simons.

Barcelona pia walionyesha uwezo mkubwa wa kurejea mchezoni, wakitoka nyuma 1-0 na kuwafunga Eintracht Frankfurt 2-1 ugani Camp Nou.

Ansgar Knauff aliweka Frankfurt mbele, lakini mabao mawili ya vichwa kutoka kwa Jules Kounde kutokana na asisti za Marcus Rashford na Lamine Yamal, yaliwapa wenyeji ushindi muhimu.

Kuingia kwa Rashford kipindi cha mapumziko kulibadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo.

Matokeo, Desemba 9:

Kairat 0-1 Olympiacos,

Bayern 3-1 Sporting,

Atalanta 2-1 Chelsea,

Monaco 1-0 Galatasaray,

Union Saint-Gilloise 2-3 Marseille,

PSV Eindhoven 2-3 Atletico Madrid,

Barcelona 2-1 Eintracht Frankfurt,

Inter Milan 0-1 Liverpool,

Tottenham 3-0 Slavia Prague