Junior Starlets wakosea adabu Uganda safari ya kuingia Kombe la Dunia U17
KENYA Junior Starlets walianza kampeni ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 kwa kishindo, wakichabanga Uganda Teen Cranes 2-0 mechi ya mkondo wa kwanza wa raundi ya pili ya mchujo uwanjani Nakivubo Hamz jijini Kampala, Uganda, Jumamosi.
Mechi ya marudiano ni Machi 16 katika uga wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi.
Mshindi kwa jumla ya mabao atasonga mbele kukabiliana na Cameroon au Ethiopia mwezi ujao katika raundi ya tatu na ya mwisho ya mchujo.
Matokeo ya Jumamosi yanamaanisha Starlets sasa wako guu moja ndani ya raundi ya tatu na watahitaji sare yoyote au wakaze buti ili kuzuia kutofungwa zaidi ya mabao matatu.

Kombe la Dunia U17 litafanyika bara Afrika kwa mara ya kwanza kabisa litakapoandaliwa nchini Morocco kuanzia Oktoba 17 hadi Novemba 8 mwaka huu.
Wachezaji saba kati ya 11 walioanza jijini Kampala walicheza makala yaliyopita ya Kombe la Dunia yaliyofanyika Jamhuri ya Dominica mwaka jana. Hao ni kipa Velma Abwire, mabeki Lorine Ilavonga, Jenevive Mithel na Ochaka, kiungo Lindy Weey, na washambuliaji Halima Imbachi na Joan Ogola.
Aidha, beki Judith Nandwa, kiungo Anita Bakaria na wavamizi Brenda Achieng na Edinah Nasipwondi walichezea Starlets kwa mara ya kwanza.
Licha ya kutawala dakika 30 za kwanza, Starlets walipoteza nafasi kadhaa nzuri kujiweka kifua mbele. Hata hivyo, jitihada zao zilizaa matunda walipopata bao la kwanza dakika ya 36 baada ya Nasipwondi kuwachenga mabeki wa Uganda, kutokana na pasi ndefu ya nahodha wa zamani Elizabeth Ochaka.
Katika muda wa nyongeza dakika ya 46 waliongeza bao la pili kupitia Ogola aliyesukuma shuti ya mbali wavuni kipa Hairu Nabbosa akishindwa kulizuia. Bao hilo lilitokana na pasi ya Weey kutokea katikati mwa uwanja.
Cheche awatuliza boli
Vigoli hao wanaonolewa na kocha Mildred Cheche hawakucheza mchujo wa raundi ya kwanza baada ya kupewa tikiti ya moja kwa moja hadi raundi ya pili pamoja na Zambia na Nigeria, kwa sababu timu hizo tatu zilicheza Kombe la Dunia 2024. Uganda iliingia raundi ya pili kufuatia ushindi wa jumla wa magoli 18-0 dhidi ya Namibia mwezi Januari.
“Lengo letu lilikuwa alama tatu la sivyo angalau tutoke sare au alama tatu, na tulitimiza hilo. Lakini mabao mawili hayatoshi kutufanya tulaze damu. Kupiga hatua tunastahili sasa kufunga mengine mengi mchuano wa marudino nyumbani na pia kurekebisha baadhi ya makosa tuliyofanya katika mechi hii,” alisema Cheche baada ya gozi la Jumamosi.