Kakamega High tayari kuandaa mashindano ya shule za upili nchini
MAANDALIZI ya mashindano ya kitaifa ya Shirikisho la Michezo ya Shule za Upili Nchini Kenya (KSSSA) yamepamba moto mjini Kakamega kipenga cha mwanzo kikitarajiwa kupulizwa Jumamosi.
Viwanja vimekaguliwa huku timu zikiendelea na mazoezi makali tayari kwa mashindano hayo ya wiki nzima yatakayoanza Julai 26 hadi Agosti 2.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa KSSSA Kanda ya Magharibi, Quinto Musungu, viwanja vyote vitakavyotumika tayari vimekaguliwa na viko katika hali nzuri.
“Tunahakikisha kila kitu kiko sawa kulingana na mipango yetu ya kuandaa mashindano. Timu zote zinatarajiwa kuwasili kufikia Julai 26 kabla ya uzinduzi rasmi kesho yake katika Shule ya Upili ya Kakamega,” alisema Musungu mnamo Jumatatu.
Kauli yake inajiri baada ya mwanafunzi wa kidato cha tatu kuaga dunia ghafla wakati wa mashindano ya soka baina ya madarasa katika shule hiyo ya Kakamega High. Polisi wanafanya uchunguzi kubaini kiini cha kifo hicho cha ghafla.

Mitanange ya shule za upili wikendi hii itahusisha mechi kali kutoka kwa timu bora katika soka, voliboli, mpira wa pete (netiboli), mpira wa vikapu kwa wachezaji watatu kila upande (3×3), raga ya wachezaji saba kila upande, na tenisi.
Mabingwa watetezi wa kitaifa Butere Girls na Madira Girls watatetea heshima ya Kanda ya Magharibi kwenye soka ya wasichana, huku timu maarufu ya The Scorpions kutoka Musingu Boys ikiongoza upande wa wavulana.
Washindani wapya Bishop Sulumeti Girls kutoka Lugari watawakilisha kanda kwenye voliboli ya wasichana, nao Malava Boys waliowahi kushinda taji la kitaifa watalenga kurejesha ufalme wa voliboli nyumbani.
Katika michezo mingine, Bukokholo itapeperusha bendera ya kanda kwenye netiboli, huku Sirakalu Secondary na Tigoi Girls zikishiriki vikapu vya wasichana. Sigalame Boys na St Peter’s Mumias zitawania taji la wavulana kwenye mpira wa vikapu.

St Peter’s Mumias, Bungoma High, Musingu Boys na Koyonzo Boys watawakilisha kanda hiyo ya Magharibi katika raga, huku mabingwa watetezi kitengo cha wasichana St Maurice Mwira pamoja na Eregi Girls, Madira Girls na Kimobo Girls pia wakishiriki.
Shule limbukeni Agai Secondary School itaongoza Kanda ya Nyanza kuwania taji la soka ya wavulana huku Kobala Mixed wakiwakilisha wasichana.
St Mary’s Yala na Sigoti Complex Girls zitawania taji la raga, huku mabingwa wa zamani wa netiboli kitaifa Oyugi Ogango Girls High wakiendea taji hilo tena.
Gogo Secondary watakuwa wakisaka ubingwa wa voliboli ya wavulana, huku Nyakongo Secondary wakivaana katika voliboli ya wasichana.
St Joseph’s Boys High wataongoza mavizio ya soka ya wavulana kutoka Bonde la Ufa, huku Nasokol Girls kutoka Pokot Magharibi wakipigania taji la wasichana.

St Joseph’s Girls Kitale watashiriki netiboli huku Bwake Boys, St Joseph’s Girls na Itigo Girls zikiwakilisha Bonde la Ufa katika raga.
Mabingwa wa zamani wa kitaifa na Afrika Mashariki wa voliboli Cheptil Boys wataongoza mawindo ya Bunde la Ufa kwa upande wa wavulana, nao Kesogon Secondary watabeba matumaini katika kitengo cha wasichana.
Kwa mujibu wa Musungu, raga itachezwa katika uwanja wa Kakamega Bull Ring, huku soka ikifanyika katika viwanja vitatu shuleni humo pamoja na Mukumu Boys.
Voliboli, netiboli, tenisi ya mezani, na badminton zitachezwa katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Muliro (MMUST), huku badminton ikifanyika pia katika shule ya upili ya Kakamega High.
Kaunti ya Kakamega pia itakuwa mwenyeji wa makala ya 22 ya Michezo ya Shule za Upili za Afrika Mashariki (FEASSSA) mnamo Agosti 14-25.
-Imetafsiriwa na Geoffrey Anene