Karura Community FC yazindua uzi mpya
Karura Community FC imezindua uzi mpaya kuelekea msimu mpya wa Ligi ya Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Kanda ya Kati, ambao unatarajiwa kuanza tarehe 25 mwezi huu.
Ukanda huo ambao unajumuisha kaunti ya Murang’a, Nyeri, Laikipia, Kirinyaga na Kiambu inazidi ya timu 100 amabzo zinashiriki ligi hiyo.
“Tutawasaidia vijana kusalia shuleni na kutimiza ndoto zao. Tutawasaidia vijana kuendeleza vipaji vyao, kujijenga na kuwa sehemu ya jamii, na kutengeneza fursa kwa ajili ya maisha yao ya baadaye,” alisema Mkurugenzi Mtandaji wa klabu hiyo Gitonga Kigo.
Nae kocha wa timu hiyo Benson Kamau aliongezea akisema , “Chini ya timu ya wakubwa, tuna watoto zaidi ya mia moja. Tuna timu ya walio chini ya umri wa miaka 7, timu ya walio chini ya umri wa miaka 15, na timu ya wakubwa. Klabu hii imetuleta pamoja ili kuwapa watoto hawa fursa maishani, ni jambo la kutia moyo,”.”
Hatua hii inalenga kuimarisha soka ya mashinani na kukuza malengo ya klabu hiyo.
Uzinduzi huo uliwezeshwa na wadhamini wa klabu hiyo, Karura Community Sacco na Pesipesa Limited, ambao ushirikiano wao unatarajiwa kusaidia shughuli za klabu na kuimarisha maendeleo yake ndani na nje ya uwanja.
Klabu hiyo pia ilitambua juhudi za wachezaji wake wanaoshiriki ligi ya kanda, ikisifu kujituma, nidhamu na bidii yao katika kuendeleza malengo ya timu.
Kwa mujibu wa klabu hiyo, ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kujenga mfumo endelevu wa soka, kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha uhusiano wake na jamii.
Karura Community FC ilimaliza katika nafasi ya tano msimu uliopita, ikiwa imekosa nafasi ya kupandishwa hadi Ligi ya Daraja la Pili kwa tofauti ya alama sita pekee.
Klabu hiyo sasa inalenga kufanya vizuri zaidi msimu huu huku ikitarajia kuimarisha kikosi chake na kutumia ushirikiano wa wadhamini kufanikisha malengo yake.
Ligi ya Kanda ya Kati inatarajiwa kuanza Oktoba 25, huku Karura Community FC ikitarajia kutumia jezi hiyo mpya kama ishara ya mwanzo mpya na azma ya kupigania nafasi ya kupanda daraja.