Dimba

KCB na Kabras kutifuana nusu-fainali ya Enterprise Cup

Na GEOFFREY ANENE March 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAFALME wa zamani wa kipute cha raga ya wachezaji 15 kila upande cha Enterprise Cup, KCB RFC, watafufua uhasama na mabingwa watetezi Kabras Sugar katika nusu-fainali itakayopigiwa uwanja wa ASK Showground mjini Kakamega, Jumamosi.

Wanabenki wa KCB waliokamilisha msimu huu wa kawaida wa Ligi Kuu (Kenya Cup) kwa kupoteza mikononi mwa Kabras 25-17 ugani humo mnamo Machi 8, watalenga kulipiza kisasi kwani pia walisalimu amri 32-20 katika fainali ya Enterprise Cup 2024.

KCB wanafukuzia taji lake la sita la Enterprise Cup, lakini la kwanza tangu mwaka 2017. Vijana wa kocha Oliver Mang’eni waliibuka washindi mwaka 2004, 2007, 2015, 2016 na 2017.

James Olela wa Kabras afunga trai dhidi ya KCB wakati wa fainali ya Enterprise Cup ugani RFUEA, Nairobi, mnamo 2024. PICHA | CHRIS OMOLLO

Wanasukari wa Kabras walitawala Enterprise Cup mwaka 2019, 2022, 2023 na 2024. Mang’eni amejaa motisha kuwa KCB watafanya vyema kwa kuwa wako tayari kupigania mataji msimu huu.

“Kwa muda mfupi, tumefanya mabadiliko makubwa na kuimarisha kikosi. Nimeridhishwa na jinsi vijana walicheza wikendi iliyopita licha yetu kupoteza. Mbinu zetu naona zinafanya kazi,” alitanguliza akasema nyota huyo wa zamani wa Kenya Shujaa na Simbas aliyechukua usukani kutoka kwa Curtis Olago kabla msimu 2024-2025 kuanza.

Akaongeza: Tunataka kuendelea kucheza hivi kwa sababu hatimaye naona tukirejesha KCB juu inakostahili, kushinda mataji.”

Naye nahodha Jacob Ojee alisema watapambana kiume kuhakikisha wanafuzu kwa fainali wakilenga kunyanyua kombe hilo.

“Nafurahia kuwa vijana wanaonyesha kiu kubwa ya kutwaa mataji. Tunajitahidi sana kuona tunashinda taji. Chipukizi walioungana nasi wameleta mwelekeo mpya na matumaini yangu ni kuwa tutazoa mataji kufikia mwisho wa msimu huu,” akaeleza Ojee.

Wachezaji wa Nondies wamkaba Beldad Ogeta wa Menengai Oilers mechi ya Kenya Cup katika uwanja wa ASK Nakuru jijini Nakuru, hapo Februari 2025. PICHA | BONIFACE MWANGI

Nusu-fainali nyingine itakuwa kati ya Menengai Oilers na Nondescripts.

Kabras na KCB walifuzu moja kwa moja kushiriki nusu-fainali ya Kenya. Wanasubiri washindi wa tiketi mbili zilizobaki kati ya Nondescripts vs Kenya Harlequin, na Menengai Oilers vs KU Blak Blad.