Dimba

KCB yaongeza makali ya klabu zake za raga, soka, voliboli na chesi

Na GEOFFREY ANENE July 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Benki ya KCB imeboresha vikosi vya timu zake za raga, soka, voliboli na chesi Julai 24, 2025 kabla ya msimu 2025-2026 kuanza.

KCB ilianzisha mchakato huo kwa lengo la kudhibiti mashindano ya kitaifa na kikanda katika fani mbalimbali.

Kutoka kwa usajili wa wachezaji wa hadhi ya juu hadi mabadiliko ya benchi la kiufundi, KCB imeonyesha kujitolea kwa dhati kwa ubora wa michezo na inaziandaa timu zake kwa msimu mpya ikitarajiwa kupata ushindi.

Maboresho hayo yameambatana na uzinduzi wa sare mpya za mechi kwa timu za raga, soka na voliboli. Sare hizo, ambazo zimebuniwa upya na kubeba nembo mpya, pia zitauzwa kwa mashabiki ili kuimarisha utambulisho wa timu na kuongeza ushirikiano wa karibu na mashabiki.

Katika raga, mabingwa mara nne wa ligi kuu ya Kenya Cup, KCB RFC, ambao wako chini ya kocha wa muda Dennis Mwanja, wamenunua wachezaji wapya Kelvin Ochieng kutoka Northern Suburbs, Collins Oduor (Nondescripts), Biko Brandon, Joseph Wanja, na Ian Oduor (Kabras Sugar), nahodha wa timu ya taifa ya Kenya Shujaa George ‘Japolo’ Ooro, pamoja na John Aswani, na Steven Osumba (Strathmore Leos), Mike Oduor (Daystar Falcons) na Clyde Kimaya na Haffith Muhammad (South Coast Pirates).

Katika soka, KCB FC inayotiwa makali na kocha mpya Robert Matano, imesajili wachezaji wenye uzoefu kama Humphrey Mieno, Gideon Were, Rowland Makati, Kelvin Injili, Arnold Muhanji, Fortune Omoto, Amatton Samunya, Josephat Andafu na Tedja Wanumbi.

Usajili huu unaonyesha dhamira ya KCB FC kupigania ubingwa kwenye Ligi Kuu. Klabu pia imeajiri John Njogu kama kocha wa mazoezi katika benchi la ufundi.

“Tunaamini kuwa mafanikio uwanjani huanzia kwa uwekezaji wa kimkakati nje ya uwanja. Mabadiliko haya hayaangazii tu utendaji, bali yanaonyesha dhamira yetu ya muda mrefu ya kuinua vipaji, kukuza michezo ya Kenya, na kuhusiana kwa undani zaidi na mashabiki wetu,” alisema Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa KCB, Rosalind Gichuru.

Katika voliboli, KCB imekaribisha kikosini seta wa kimataifa Esther Mutinda, ambaye alikuwa muhimu katika ushindi wao wa dhidi ya Kenya Pipeline na kutajwa kuwa seta bora wa mashindano.

Nguvu ya KCB katika voliboli inaonekana pia kupitia uteuzi wa wachezaji saba wa timu hiyo kwenye kikosi cha taifa kitakachoshiriki Mashindano ya Dunia nchini Thailand kuanzia Agosti 22 hadi Septemba 7. Wachezaji hao ni Marlene Tata, Juliana Namutira, Belinda Barasa, Deborah Jesang, Fridah Boke,
Pauline Chemutai na Shirleen Maywa.

Katika mchezo wa chesi, KCB haionyeshi dalili zozote za kupunguza kasi. Timu hiyo inaongoza Ligi Kuu kwa alama 25 na inaelekea kushinda taji lake la tisa. Hivi majuzi, wanabenki wa KCB walionyesha uwezo wao kwenye mashindano ya chesi ya Kitale Open, wakitawala kitengo cha mashirika.