Dimba

Kenya yenye wachezaji 10 yaikaba Angola Kundi A CHAN

Na CECIL ODONGO August 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KENYA iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani Alhamisi iliagana sare ya 1-1 na Angola kwenye mechi ya pili ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024).

Mechi hiyo iliyogaragazwa uga wa MISC Kasarani,  ilikuwa na drama ya aina yake.

Hii ni kwa sababu muda wa ziada Angola ilipata bao na kusherehekea kwa kishindo lakini likaondolewa kwa sababu mchezaji wao alikuwa ameotea.

Angola walichukua uongozi kupitia Jaoquim Paciencia dakika ya sita baada ya kupokezwa pasi na Beni Mukendi.

Pia bao hilo lilichangiwa na masihara ambayo yalifanywa langoni na kipa Bryine Omondi.

Hata hivyo, vijana wa nyumbani walijinusuru kupitia penalti ya Austin Odhiambo dakika ya 12 baada ya kukanyagwa kwake ndani ya kijisanduku.

Hili lilikuwa bao la pili kwa Austin, kiungo wa Gor ambaye pia alifungia Kenya katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Jumapili.

Ilibidi Kenya isalie na wachezaji 10 uwanjani katika dakika ya 21 baada ya Marvin Nabwire kupewa kadi nyekundu kwa kumkanyaga Paciencia nje ya kijisanduku.

Licha ya Angola kumiliki mpira kwa kipindi kirefu, haikuweza kupenya na kufunga bao la ushindi.

Dakika ya 90, Joao Kaporal aliupiga mpira wa kichwa baada ya kupokea krosi upande wa kulia na mpira ukamlemea Bryine Omondi kunyaka.

Bao hilo lilishangiliwa na Angola lakini sherehe hizo zikakatizwa baada ya refa kuangalia VAR na kuamua Kaporal alikuwa ameotea.

Kutokana na sare hiyo, wanasoka wa Harambee Stars watapata Sh500,000 jinsi walivyoahidiwa na Rais William Ruto.

Wiki hii walipokezwa Sh1 milioni kwa kuishinda DR Congo huku serikali ikitoa jumla ya Sh42 milioni.

Kenya ipo kileleni mwa Kundi A kwa alama nne baada ya mechi mbili, huku Morocco ikiwa ya pili kwa alama mbili.

Morocco itacheza mechi yake ya pili Jumapili ambapo itavaana na Kenya katika uga huo huo wa Kasarani.

DR Congo ni ya tatu kwa alama tatu ikiwa imecheza michuano miwili pia.

Angola ina alama moja baada ya mechi mbili kisha Zambia inavuta mkia bila alama yoyote.