Kocha mpya wa Chelsea Liam Rosenior aahidi raha tupu
LONDON, UINGEREZA
KOCHA mpya wa Chelsea Liam Rosenior ameahidi kuleta raha Stamford Bridge akisema kwamba, anajiunga na timu ambayo “ina njaa kushinda”.
Rosenior, 41, alitangazwa rasmi na The Bluez Jumanne, Januari 6, 2026, baada ya kusaini mkataba wa miaka sita, akitokea Racing Club de Strasbourg Alsace ya Ligi Kuu ya Daraja la Kwanza nchini Ufaransa.
“Kuna njaa ya kweli ya kushinda,” alisema. “Nitafanya niwezavyo, kila siku, ili kuisaidia timu hii kushindana na kushinda katika ngazi ya juu na kufanya kila mtu anayehusishwa na timu hii kujivunia kuwa sehemu ya klabu ya Chelsea.”
Aliongezea akisema, “Ninaamini sana katika kufanya kazi pamoja. Maadili hayo yatakuwa katika kila kitu tunachofanya. Yatakuwa msingi wa mafanikio yetu. Kuaminiwa na jukumu hili kunamaanisha kila kitu kwangu. Nawashukuru wote ambao waliniamini na kuchagua kufanya kazi hii,” Rosenior aliambia Chelsea jana.
Pia, alituma ujumbe kwa mashabiki.
“Ninataka mashabiki wetu wajivunie timu hii na kila mchezo tunaocheza. Wao ndio roho ya klabu hii kubwa yenye ya historia kubwa. Nina hamu ya kukutana nanyi.”
Klabu ya Chelsea ilitangaza rasmi ujio wake jana.
“Klabu ya Soka ya Chelsea inafuraha kutangaza uteuzi wa Liam Rosenior kama kocha mkuu wa timu ya wanaume. Mwingereza huyo amesaini mkataba na klabu ambao utamfikisha hadi 2032,” taarifa hiyo ya Chelsea ilisoma.
Akiwa mchezaji, alicheza kama beki wa pembeni na wing’a. Alichezea Bristol City, Fulham, Torquay United, Reading FC, Ipswich Town, Hull City na Brighton & Hove Albion.
Pia, aliwahi kuichezea timu ya Uingereza ya wachezaji 20 na 21 na kucheza jumla ya mechi 11 na kufunga bao moja.
Rosenior hana uzoefu mkubwa wa kunoa vilabu vikubwa. Alikuwa meneja wa muda huko Derby County mnamo 2022 na kabla ya kujiunga na Hull Novemba 2022 hadi Mei 2024. Aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa Strasbourg mnamo Julai 2024 na baadae kujiunga na Chelsea.
Anachukua nafasi ya Enzo Maresca ambaye alijiuzulu siku ya mwaka mpya.
Kibarua cha kwanza cha Rosenior kitakuwa kuongoza Chelsea katika raundi ya tatu ya Kombe la FA dhidi ya Charlton Athletic timu ya Championship.
Kocha msaidizi Callum McFarlane, ambaye alisimamia sare ya 1-1 dhidi ya Manchester City siku ya Jumapili, atasimamia mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Fulham leo ingawa Rosenior atatazama na mashabiki.
Ratiba ya mechi za leo
Fulham vs Chelsea (10:30 pm)
Crystal Palace vs Aston Villa (10:30 pm)
Bournemouth vs Spurs (10:30 pm)
Everton vs Wolves (10:30 pm)
Newcastle vs Leeds United (11:15 pm)
Brentford vs Sunderland (10:30 pm)
Manchester City vs Brighton (10:30 pm)
Burley vs Manchester United (11:15 pm)