Liverpool yasikitika na nusu mkate ya Everton, Arsenal watabasamu
VIONGOZI Liverpool wamesikitika kugawana alama na majirani Everton katika sare ya 2-2, kwenye gozi la 120 na mwisho la Merseyside ugani Goodison Park kabla ya Toffees wahamie uwanja mpya wa Bramley-Moore Dock msimu ujao.
Katika mechi hiyo ya akiba iliyoahirishwa kutoka Desemba 7, 2024 hadi Februari 12 kutokana na hali mbaya ya anga, wenyeji Everton walianza vyema Beto alipomwaga Allison Becker dakika ya 11 kutokana na pasi murwa kutoka kwa Jarrad Branthwaite baada ya frikiki.
Hata hivyo, Liverpool ilisawazisha 1-1 dakika tano baadaye kupitia Alexis Mac Allister aliyekamilisha krosi ya Mohamed Salah kwa kichwa kabla ya raia huyo wa Misri kupachika bao lake la 22 ligini kwa kuweka wageni juu 2-1 dakika ya 73.
Ni mara ya tisa Salah amefunga bao na kuchangia asisti katika mechi ya Ligi Kuu msimu huu.
Hakuna mchezaji mwingine amechangia bao na asisti katika zaidi ya mechi saba ndani ya msimu mmoja.
Beki James Tarkowski alihakikishia Everton alama alipoduwaza Reds na bao la dakika ya nane ya majeruhi.
Bao hilo lilisimama baada ya kuchunguzwa na VAR kwa muda mrefu kuona kama Abdoulaye Doucoure alikuwa ameotea.
Ni mechi tuliyotarajia itakuwa moto. Vita vilikuwa vingi. Tunasikitika sana kufungwa bao sekunde ya mwisho ya mchezo, lakini hiyo ni hali ya soka. Si rahisi kukubali matokeo haya, lakini tunayachukua na kusonga mbele. Ni motisha kwa Everton, lakini pigo kwetu
Tarkowski alikamilisha kwa ustadi pasi ya Tim Iroegbunam na kusherehekea goli lake kwa kupiga mbizi katika sehemu ya nyuma ya lango ya mashabiki wa Everton.
Sherehe zilichochea drama kipenga cha mwisho kilipopulizwa na refa baada ya wachezaji kutoka timu zote mbili kukabiliana, huku Curtis Jones (Liverpool) na Doucoure (Everton) wakilishwa kadi nyekundu.
Slot na naibu wake Sipke Hulshoff pia walionyeshwa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu.
Slot hakuanzisha mchezaji hata mmoja kutoka Uingereza katika kikosi cha kwanza cha wachezaji 11 akiweka historia mpya ya Liverpool ligini.
Liverpool sasa imepanua mwanya wa alama saba kileleni baada ya timu zote 20 kusakata michuano 24.
Everton, ambayo ina ushindi 41 dhidi ya Liverpool na kupoteza 41 pamoja na kutoka sare 38, iliingia mpepetano huo na motisha ya kuzoa ushindi mara tatu mfululizo ligini.
Chelsea waendea kisasi kwa wenyeji Brighton
Ijumaa itakuwa zamu ya Brighton (nambari 10) kualika Chelsea (nne) ugani Amex.
Brighton wameona giza mara tatu mfululizo dhidi ya Blues.
Isitoshe, Brighton wataingia mchuano huu wakiuguza vichapo vitatu mfululizo ligini msimu huu.
Seagulls walizabwa 7-0 na Nottingham Forest katika mechi iliyopita nao Chelsea walilemea West Ham 2-1.
Hata hivyo, wataingia dimbani kichwa juu baada ya kubandua wageni wao 2-1 kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Uingereza (FA Cup), uwanjani Amex mnamo Jumamosi iliyopita.