Dimba

Man City wapigia hesabu Carabao

Na MASHIRIKA December 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MANCHESTER, UINGEREZA

MANCHESTER City watakuwa nyumbani Jumatano usiku kuwaalika Brentford kwenye robo-fainali ya Carabao Cup.

Timu hizi zinajivunia kiwango kizuri kwa sasa lakini wenyeji wanapewa asilimia kubwa ya kupata ushindi baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini katika mechi ya mkondo wa kwanza ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

City wanaingia uwanjani wakijivunia ushindi wa 3-1 dhidi ya Crystal Palace katika mechi ya ligi, Jumapili.

Erling Haaland alifunga mabao mawili naye Phil Foden akafunga moja, ushindi ambao umeimarisha matumaini yao ya kutwaa taji la EPL msimu huu, wakiwa nyuma ya vinara Arsenal kwa pengo la pointi mbili pekee.

Ushindi kwa kikosi hicho cha Pep Guardiola utakuwa wa tano mfululizo katika mashindano tofauti.

City wamerejea kwa kishindo baada ya hapo awali kushindwa na Newcastle United ligini na Bayer Leverkusen kwenye Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya.

Walifuzu kwa hatua hii ya Carabao Cup baada ya kubandua Swansea 3-1 katika raundi ya nne.

Katika mechi ya leo, City wataingia uwanjani bila mastaa wanouguza majeraha- Jeremy Doku, Mateo Kovacic, Rodri, John Stones na Ryan McAidoo.

Kwenye robo fainali nyingine, Fulham watakuwa ugenini St James’ Park kukabiliana na Newcastle United.

Ni mechi ambayo kocha Eddie Howe atapanga kikosi chake bila Dan Burn anayetarajiwa kukaa nje kwa wiki sita baada ya kujerujiwa vibaya mwishoni mwa wiki.

Lakini huenda kocha huyo akamkaribisha Sven Botman, wakati Emil Krapth na Kierran Tripper wakiendelea kukaa nje hadi watakapopata nafuu.

Wakati huo huo, kocha Enzo Maresca wa Chelsea amekataa kueleza madai yake kuhusu watu aliodai wanamharibia jina kila wakati timu hiyo iposhindwa.

Kabla ya kucheza robo fainali ya Carabao Cup dhidi ya Cardiff, Maresca, 45 alidai kwamba kuna fulani kwenye uongozi wa klabu hiyo ambao hawamsaidii ipasavyo.

Maresca alitoa maoni hayo baada ya kikosi chake kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Everton.

Huku akishinikizwa ataje watu waliokuwa wakivuruga kazi yake, Maresca alisema ana jukumu la kubadilisha kikosi chake kwa sababu kinashiriki katika mashindano tofauti kwa wakati mmoja.

“Tayari nimezungumzia jambo hili na sina jingine la kuongeza. Ninaheshimu maoni ya wanahabari pamoja mashabiki lakini kuna wakati wanapita kipimo.”

Kocha huyo amekuwa akikabiliwa na shutuma za kila aina, kama ilivyoshuhudiwa Chelsea iliposhindwa kwa mabao 2-1 na Atalanta ya Italia katika pambano la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya juma lililopita.

Mbali na Manchester City, Newcastle, na Chelsea katika hatua hiyo ya Carabao, kuna Arsenal wanaowakaribisha Crystal Palace juma lijalo.