Man U wajiandaa kuzima kabisa matumaini finyu ya Arsenal ligini
JOHN ASHIHUNDU NA MASHIRIKA
MANCHESTER United watalenga ushindi watakapokabiliana na Arsenal Jumapili katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza itakayochezewa Old Trafford.
Kikosi hicho cha kocha Erik ten Hag ambacho kilishindwa 3-1 katika mkondo wa kwanza ugani Emirates kinarejea uwanjani baada kutandikwa 4-0 na Crystal Palace katika mechi iliyopita.
Wakati huo huo, Manchester City walichapa Fulham United 4-0 ugani Craven Cottage na kuipiku Arsenal kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada kukusanya pointi 85, mbili zaidi ya Arsenal ambao leo watakuwa ugenini Old Trafford kukabiliana na Manchester United.
Manchester United wanacheza mechi hii wakiwa katika nafasi ya nane jedwalini, kutokana na ushinsi mara mbili katika mechi 10 zilizopita.
Lakini ni mechi ambayo Arsenal watapigania ushindi ili waendelee kwenda sako kwa bako dhidi ya Manchester City kwenye mbio za kufukuzia ubingwa, vita ambavyo vinaonekana kwenda hadi siku ya mwisho.
Kocha Mikel Arteta anatarjiwa kuwa mtulivu katika mchezo huo baada ya kuonyeshwa kadi tano za njano, ambapo akionyeshwa nyingine, itabidi akae nje katika mechi ya mwisho dhidi ya Everton
United hawajawahi kumaliza nyuma ya 10 bora katika historia ya ligi hiyo, lakini ni miongoni mwa timu zinazowania kumaliza katika nafasi nzuri ili kufuzu kwa michuano ya Ulaya. Hata hivyo, wanaweza kufuzu kwa mechi za Europa League iwapo watashinda ubingwa wa FA Cup.
Bukayo Saka na Takehiro Tomiyasu waliokuwa wakisumbuliwa na majeraha, wamepata nafuu na tayari kucheza leo.
Kuelekea kwa mechi ya leo, kocha Ten Hag alithibitisha kwamba kiungo mshambuliaji Masson Mount hatakuwa kikosini baada ya kujeruhiwa mazoezini Alhamisi, lakini huenda Scott McTominary, Bruno Fernandes na Marcus Rashford wakarejea.
Kama kawaida, kipa Andre Onana atakuwa langoni, huku Casemiro akitarajiwa kucheza kama beki wa katikati akishirikiana na Jonny Evans, ingawa Lisandro Martinez amerejea mazoezini baada ya kutatizwa na jeraha. Aaron Wan-Bissaka na Diogo Dalot wanatarjiwa kucheza kama mabeki wa pembeni.
Fernandes na Kobbie Mainoo pamoja na Christian Eriksen wanatarjiwa kumiliki safu ya kiungo, lakini huenda Sofyan Amrabat akakosa nafasi katika kikosi hicho.
Hakuna mshambuliaji aliye katika kiwango kizuri, hivyo, huenda akina Alejandro Garnacho na Rasmus Hojlund wakaanza badala ya Antony Matheus.
Manchester City ambao ndio mabingwa watetezi wamecheza mechi pungufu kwa mechi moja huku wakisubiri kupepetana na Tottenham Hotspur na West Ham United.
Arsenal walikuwa wakiomba Fulham wawafanyie msaada kwa kushinda City au kutoka nao sare lakini dua yao haikutimika, huku mashabiki wa The Gunners wakiingiwa na wasiwasi.
Baada kumalizana na Fulham Jumamosi katika uwanja wa Etihad, City wataelekea jijini London, Jumanne kupepetana na Tottenham Hotspur.
City watamaliza msimu uwanjani Etihad dhidi ya West Ham United, siku ambayo Arsenal watakuwa nyumbani Emirates kucheza na Everton.