Maombi ya Arsenal yatuza Man United kombe la Emirates FA kwa kukomoa Man City 2-1
NA MWANGI MUIRURI
MAOMBI ya Arsenal kwa niaba ya Manchester United kabla ya mchuano wa fainali ya Emirates FA dhidi ya Manchester City yamejibiwa.
Sasa, Man United ndio mabingwa wa kombe hilo msimu huu wa 2023-24 baada ya kuikomoa Man City 2-1 ugani Wembley Jumamosi jioni.
Mabao ya Alejandro Garnacho wa umri wa miaka 19 kunako dakika ya 32 na lile la Kobbie Mainoo wa umri wa miaka 19 pia katika dakika ya 39 ndio yalibeba Man United kunyanyua taji la FA.
Bao la Jeremy Doku katika dakika ya 87 halikutosha mboga kuzuia dau la Man City kuzama.
Arsenal ikiwa na machungu ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika dakika ya mwisho baada ya Man City kukosa kuteleza, ilienda Wembley kushabikia Man United.
Hali hiyo sio ya kawaida kamwe kwa kuwa Man United na Arsenal huwa ni mahasimu wa kutaniana na ambapo hakuna humpendea mwingine mazuri ugani.
Katibu wa vuguvugu la Central4Arsenal Bw Eliud Mwaura akiwa mjini Nyeri alikuwa amesema kwamba “haki na usawa ni kuunga mkono timu ya Man United licha ya kuwa ni watani wetu wa jadi”.
Bw Mwaura alikuwa amesema kwamba busara hiyo ilichochewa na hali kwamba Arsenal, Man City, Liverpool na Aston Villa tayari wamejihakikishia kushiriki dimba la Klabu Bingwa Ulaya (Uefa) hivyo basi kuwa na haja ya timu ya Man United nayo iiingie kwa dimba la Europa.
“Baada ya timu ya Man U kukosa kutinga ndani ya saba bora katika Ligi kuu ya Uingereza (EPL) hivyo basi kujipata nje ya mitanange ya Europa, kuibuka bingwa wa FA msimu huu kutaifanya itue moja kwa moja ndani ya michuano ya Europa,” akasema.
Seneta maalum Bi Karen Nyamu licha ya kuwa shabiki sugu wa Arsenal alikuwa amesema kwamba hana la kufia lakini “hawa watani wetu wa Man U wajikakamue angalau waangukie mfupa na makombo ya Ulaya”.
Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro alisema kwamba “kwa sasa sijui mjadala ni wa nini ikizingatiwa kwamba sisi hutwaa ushindi tukipenda na kutwaa ushindwe bado tukipenda”, sasa alisema kwamba “sisi ni mabingwa pasipo kujisumbua na kura za maoni za awali”.
Bw Nyoro alisema ya kwamba “kipenga cha mwisho kimeangazia sura yetu kamili kwamba sisi huzua matokeo kwa hiari na raha zetu”.
Bw Mwaura alisema kwamba mashabiki wa Liverpool na Chelsea walikuwa wameungana kuombea Man United kilio cha FA guuni la Man City “lakini sisi kama Arsenal daima hatutawahi kujihusisha na ukatili wa kumponda vibonde aliye chini”.
Alisema kwamba Man United iliingia ugani ikiwa sawa na jamii ya wasiobahatika “na maombi yetu ya haki na usawa kwa Mungu wetu yamewajalia ushindi ndio hata wao wawe na la kupigia mdomo wakijiandaa kushiriki dimba la Europa”.