Dimba

Maradhi ya ghafla yakosa kuzuia Arsenal kufinya Brentford

Na JOHN ASHIHUNDU January 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LONDON, Uingereza

NUKSI ya maradhi ya ghafla katika kambi ya Arsenal haikuweza kuzuia wanabunduki hao kufungua mwaka kwa kuendeleza ukatili dhidi ya timu jirani kutoka jijini London baada ya kutoka nyuma na kulipua Brentford 3-1 ugani Gtech, Jumatano.

Kocha Mikel Arteta alifichua kuwa maandalizi ya Arsenal yalitatizwa na mkurupuko wa virusi katika kikosi chake.

Nyota kadhaa wa Arsenal walilemewa na ugonjwa huo siku ya kuamkia mechi hiyo ya 19.

Mshambulizi wa Ujerumani, Kai Havertz alirejeshwa nyumbani akiwa mgonjwa, naye kiungo wa Uingereza Declan Rice alianza mchuano kutoka kwenye benchi katika kipindi cha pili.

Hii ni mara ya kwanza tangu Havertz ajiunge na Arsenal kutoka Chelsea mwaka 2023 kukosa mechi kwa sababu ya ugonjwa ama jeraha.

Nahodha Martin Odegaard anasemekana kutatizwa na virusi hivyo kabla ya mechi kung’oa nanga na ingawa alianza mchezo, alifanya kosa lililosababisha Bryan Mbeumo kuweka Bees juu 1-0 dakika ya 13 kabla ya kupumzishwa dakika ya 88 na nafasi yake kutwaliwa na Jorginho.

Hata hivyo, Arsenal walijituma vilivyo na kujirejesha katika vita vya kuwania taji kwa kushinda mechi hiyo kupitia mabao ya Gabriel Jesus (dakika ya 29), Mikel Merino (50) na Gabriel Martinelli (53).

“Ugonjwa uliathiri wachezaji ndani na hata nje ya uwanja,” Arteta alisema baada ya Arsenal kuchupa hadi nafasi ya pili kutoka nambari tatu na kupunguza mwanya kati yake na Liverpool hadi alama sita, ingawa viongozi hao wana mechi moja mkononi.

“Si kitu cha kutia hofu sana. Hata hivyo, hali haikuwa shwari. Kai hakuwa anahisi vyema kabisa. Alikuwa na dalili za wazi kwa hivyo tuliamua arejee nyumbani,” akaeleza Arteta anayetumai kuwa hali itaimarika wakati wa mpepetano dhidi ya Brighton ugani Amex hapo Jumamosi.

Ushindi dhidi ya Brentford uliifanya Arsenal kuwa timu pekee iliyovuna alama nyingi katika debi za London msimu huu (14) huku Brentford na Crystal Palace zikiwa zimezoa alama chache kabisa (nne).

Arsenal wana kibarua kigumu cha mechi tisa mwezi huu.

Baada ya Brentford, vijana wa Arteta watalimana na Brighton (Januari 4), Tottenham (Januari 15), Aston Villa (Januari 18), Wolves (Januari 25) ligini, Newcastle (Januari 7, Carabao Cup), Manchester United (Januari 12, FA Cup) kisha Dinamo Zagreb (Januari 22) na Girona (Januari 29) kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya.