Dimba

Maresca ala makasi Chelsea

Na MASHIRIKA January 1st, 2026 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kunoa Chelsea kwa miezi 18, kocha Enzo Maresca ametemwa na klabu hiyo kutokana na msururu wa matokeo mabaya na tofauti za ndani kwa ndani na wakuu wa klabu.

Enzo alijiunga na The Blues mnamo Juni 2024, kwa mkataba wa miaka mitano akichukua nafasi ya Mauricio Pochettino.

Awali, alikuwa msaidizi wa Pep Guardiola huko Man City. Alikuwa ameondoka Etihad kujiunga na Leicester mnamo 2023, ambako alishinda taji la Championship.

Chelsea katika taarifa jana ilisema: “Klabu ya Chelsea na kocha mkuu Enzo Maresca wamekatiza mahusiano. Katika kipindi chake katika klabu hii, Enzo aliongoza timu hii kufanikiwa katika Ligi ya UEFA na Kombe la Dunia la Klabu la FIFA. Mafanikio hayo yatabaki kuwa sehemu muhimu ya historia ya hivi karibuni ya klabu, na tunamshukuru kwa mchango wake kwa klabu.”

Muitaliano huyo amiacha timu hiyo ikiwa ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 30, alama 15 nyuma ya vinara Arsenal.

Blues wameshinda mara moja katika mechi zao saba za mwisho za EPL. Wameshinda jumla ya mechi nane, wakaandikisha sare sita na kupoteza mara sita.

Mechi ya mwisho ya Enzo ilikuwa sare ya 2-2 Jumanne jioni nyumbani dhidi ya Bournemouth ambapo, alikosa mahojiano na wanahabari baada ya sare hiyo na kumwacha msaidizi wake Willy Caballero kufanya mahojiano hayo.

“Enzo hajisikii vizuri,” alisema Caballero. “Hakuwa anajisikia vizuri siku mbili zilizopita lakini bado alifanya mazoezi. Nilichukua nafasi yake tu kufafanua kwamba hajisikii vizuri vya kutosha kufanya mambo mengine ambayo meneja anapaswa kufanya, kwa hivyo niko hapa kumwakilisha.”

Hata hivyo, baada ya mechi hiyo, kulikuwa na ripoti za vuta ni kuvute kati yake na viongozi wa klabu hiyo.

Chelsea wanarejea uwanjani Jumapili ugenini dhidi ya Manchester City, hii ikiwa mechi ya kwanza kati ya mechi tisa katika mashindano manne Januari hii.

Wanatarajia kutangaza kocha mkuu mpya katika siku chache zijazo, huku Liam Rosenior akieleweka kuwa mmoja wa wagombea wachache ambao watazingatiwa kuchukua nafasi ya Enzo.

Rosenior ni meneja raia wa Uingereza na anahudumu kama kocha mkuu wa klabu ya Ligue 1, Strasbourg. Hapo awali katika kazi yake, alicheza kama beki wa timu ya U23 ya Brighton and Hove Albion.

Kiungo wa zamani wa Chelsea Cesc Fabregas pia amehusishwa na nafasi hiyo huku bosi wa zamani wa Barcelona Xavi akiwa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi hiyo.

Meneja wa Crystal Palace Oliver Glasner pia amehusishwa na uhamisho wa kuenda Stamford Bridge baada ya kufanya kazi ya kuvutia huko Selhurst Park, ambapo alishinda Kombe la FA msimu uliopita.