Dimba

McCarthy asifiwa kujumuisha vijana 5 wa pwani kikosi cha Harambee kombe la CHAN

Na ABDULRAHMAN SHERIFF July 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WASHIKA dau na mashabiki wa soka wa sehemu mbalimbali za Kanda ya Pwani wamempongeza kocha wa Harambee Stars, Benni McCarthy kwa kujumuisha wachezaji watano kutoka Pwani kwenye kikosi chake kinachojiandaa kwa mashindano ya CHAN.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) tawi la Kaunti ya Mombasa, Alamin Mohamed amempongeza McCarthy kuwa mkufunzi mwenye kutambua vipaji vya wachezaji aliowachaguwa bila ya kuchagua wametoka timu gani.

“Hatuna budi kumpa heko mkufunzi wa Harambee Stars kuwachagua wanasoka watano kutoka Kanda ya Pwani kwa kikosi chake kitakachoshiriki mashindano ya CHAN. Amewapa moyo wanasoka wengine wa Pwani kuwa wana nafasi katiksa timu yao ya taifa,” akasema Mohamed.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Cosmos FC Aref Baghazally amesema uteuzi alioufanya McCarthy ndio bora zaidi kwa miaka kadhaa na akaeleza imani yake wanasoka wote watano kutoka Pwani kubakia katika kikosi kitakachoshiriki dimba hilo.

Shabiki wa Bandari FC, Henry Mwaidoma wa Mwatate anasema ni fahari kubwa kwa wanasoka wote wa Pwani kutokana wenzao watano kuitwa kikosi cha timu ya taifa.

Wachezaji hao ni Beja Nyamawi, Mohammed Siraj, David Sakwa, Farouk Shikalo na Swaleh Pamba

“Huyu ndiye mkufunzi anayehitajika kuipa ushindi Kenya ambao umekosekana miaka mingi,” akasema Mwaidoma.

Sarah Karisa wa Kilifi anasema mkufunzi kama McCarthy anahitajika pia kusimamia timu ya Harambee Starlets ambayo mara zote imekuwa ikichaguwa wanasoka kutoka sehemu nyingine na kutowapa fursa wachezaji wa Pwani.

“Ningeomba FKF imkumbuke kocha Joseph Oyoo ambaye miaka mingi ameweza kuzisaidia timu kadhaa zikiwemo Shimanzi Railways, Soliwodi, Mombasa Olympic na hata shule kadhaa kutoa wachezaji wazuri ambao wengineo wanacheza soka ya kulipwa ng’ambo,” akasema Sarah.