McCarthy: Nina mbinu ya kuangusha Angola leo tuwike kwa ushindi wa pili
KOCHA wa Harambee Stars Benni McCarthy amejinaki kuwa amevumbua mbinu ya kupiga Angola leo kwenye mechi ya pili ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji Wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024).
Kenya itakuwa ikivaana na Angola kuanzia saa moja usiku leo katika uga wa Kitaifa wa Kasarani.
Harambee Stars ilishinda mechi ya kwanza mnamo Jumapili ilipoilaza Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) 1-0 katika uga huo huo wa Kasarani.
Jumatano, McCarthy alisema yupo tayari kufanya juu chini kuhakikisha kuwa Kenya inashinda mechi ya leo na kujiweka pazuri kufuzu hatua ya robo fainali.
Angola ni mabingwa wa COSAFA (Kipute kinachoshirikisha mataifa ya Kusini mwa Afrika) na licha ya kupigwa 2-0 na Morocco, ilionyesha mchezo mzuri pamoja na kwamba inaelekea mechi ya leo kwa kisasi cha juu.
“Najua wanacheza mfumo wa 3-4-3 ambao ni wa kuvamia na kulinda wakati huo huo. Hata hivyo, hatuna wasiwasi na tunajua njia tutakayotumia kuwakabili,” akasema McCarthy.
Kocha huyo hata hivyo, aliongeza kuwa huenda fowadi Masud Juma akakosa mechi hiyo baada ya kupata jeraha akiwa mazoezini.
“Katika mechi dhidi ya DR Congo, tulishambulia na ilikuwa ya kwanza kwa wachezaji wengi katika kikosi changu. Sasa angalau wana ujasiri wa kuwakabili wapinzani,” akaongeza.
Kocha huyo aliashiria kuwa kutakuwa na mabadiliko machache tu kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya DR Congo.
Kocha huyo alimpongeza kiungo wake Manzur Okwaro ambaye anachezea KCB kutokana na jinsi alivyongáa katika mchezo dhidi ya DR Congo na jinsi atakavyomtumia kwenye mechi ya leo.
“Sisi tunalenga kuwapa presha zaidi na nina hakika kuwa Manzur akiwa na mpira, basi wanasoka wengine hupata nafasi ya kukimbia mbele na kuvamia. Angola ni timu nzuri lakini sisi pia tutakuwa tukicheza,” akasema McCarthy.
Kocha wa Angola Pedro Gonvalves alisema kuwa hana majeraha yoyote katika kikosi chake na wako tayari kupambana na Kenya.
“Tunajua tuko kwenye kundi gumu na mabingwa wawili wa zamani. Licha ya kupigwa na Morocco, mashindano yetu sasa yanaanzia Kenya, wako nyumbani , wana mashabiki ila sisi lengo letu ni kupata ushindi,” akasema Pedro.