Dimba

Mkenya aumwa na mbwa Riadha za Dunia nchini India

Na GEOFFREY ANENE October 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KOCHA wa mbio fupi wa Kenya, Dennis Mwanzo, amesimulia masaibu yake baada ya kung’atwa na mbwa mmoja kati ya wengi wanaozurura katika uwanja wa Jawaharlal Nehru mjini New Delhi, India, alipokuwa akimhudumia mwanariadha.

Tukio hilo limeibua hofu kubwa kwani wanariadha na maafisa mbalimbali wamekuwa wakilalamika kuhusu visa vya kuumwa na mbwa wakati wa Riadha za Dunia za Walemavu zilizofanyika Septemba 27 hadi Oktoba 5.

Nchini India, visa vya kung’atwa na mbwa vinasemekana kuwa tatizo la kiafya la kawaida, ambapo tafiti zinaonyesha kuwa ni chanzo kikuu cha maambukizi ya kichaa cha mbwa.

Kenya iliingiza wanariadha 24 kushiriki katika makala hayo ya 12 yaliyohusisha zaidi ya wanariadha 2,000 kutoka nchi 100.

Sheila Wanyonyi na Nancy Chelangat walishindia Kenya medali. Wanyonyi alipata fedha katika kitengo chake cha kurusha mkuki F13 kwa rekodi mpya ya Afrika ya mita 38.63, huku Chelangat akitwaa fedha katika mbio za mita 1,500 T11. Wanyonyi aliimarisha rekodi yake ya awali ya 35.05m aliyoweka mwaka 2024.

Brazil iliongoza jedwali la medali na kufuatiwa na China na Poland.