Dimba

Msauzi Benni McCarthy apokezwa mikoba ya Harambee Stars, lengo likiwa kufuzu ‘World Cup’

Na JOHN ASHIHUNDU March 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BENNI McCarthy kutoka Afrika Kusini ndiye kocha mpya wa timu ya taifa ya Harambee Stars, akichukuwa nafasi ya Francis Kimanzi aliyekuwa kocha wa mpito baada ya Engin Firat raia wa Uturuki aliyejiuzulu mwishoni mwa mwaka uliopita.

Nyota huyo wa zamani aliyechezea Manchester United, Blackburn Rovers na West Ham United kwenye Ligi Kuu ya Uingereza amesaini mkataba wa miaka miwili kuinoa Stars hadi 2027.

Maarufu kama “Zulu Warrior” straika huyo mstaafu anafahamika kwa kusaidia FC Porto kutwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya chini ya Jose Mourinho mnamo 2004.

Jukumu la kocha huyo mwenye umri wa miaka 47 ni kuongoza Stars dhidi ya Gambia na baadaye Gabon kwenye mechi za mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Dunia mwezi huu.

Ivory Coast wanaongoza msimamo wa Kundi hilo la F kwa pengo la pointi tano dhidi ya Kenya, lakini Stars wamebakisha mechi tano.

Mshindi wa kundi atafuzu moja kwa moja kwa fainali hizo za Kombe la Dunia, wakati timu nne zitakazomalia katika nafasi za pili kutoka kila kundi zikifuzu kwa mchujo wa mwisho wa kufuzu.

Kenya itaandaa kwa pamoja fainali za 2027 Afcon na Tanzania na Uganda lakini haikufuzu kwa fainali za mwaka huu zitakazofanyika nchini Morocco.

McCarthy aliichezea Afrika Kusini mara 80 na kuifungia kwenye Kombe la Dunia mnamo 1998 na 2002.