Dimba

Msimu mwingine Arsenal kuwa kileleni Krismasi ila misimu ya nyuma hawakushinda taji

December 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MSIMU wa huu wa 2025/26 ni msimu wa tano ambao Arsenal itakuwa kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) siku ya Krismasi.

Hili lilitokea msimu wa 2002/03, 2007/08, 2022/23 na 2023/24 na misimu hiyo yote, Gunners hawajafanikiwa kushinda taji lolote katika misimu minne iliyopita.

Penalti ya Mswidi Viktor Gyokeres katika mechi tano msimu huu, liliwahakikishia Arsenal ya Mikel Arteta ushindi wao wa 12 msimu huu Jumamosi usiku Ugani Hill Dickinson.

Ushindi huo uliwafanya kuendelea kusalia kileleni mwa jedwali na alama 39 baada ya mechi 17.

Waliokuwa pungufu

“Nimefurahi sana, ni mahali pagumu sana kuja na kupata alama. Lazima niseme, ni uwanja mzuri waliojenga. Tulijua itakuwa mechi ngumu sana,” alisema Arteta baada ya ushindi huo.

Aliongezea akisema, “Katika kipindi cha pili tulipaswa kufunga bao la pili au la tatu ili kuwa na utulivu zaidi. Hatukufanya hivyo na dhidi ya timu ya aina hii inaweza kuwa na wasiwasi.”

Mwenzake wa Everton David Moyes alionyoosha kidole cha lawama kwa mchezaji wake Jake O’Brien ambaye alisababisha penalti hiyo.

“Sidhani kama Arsenal walitupa wakati mgumu kabla ya penalti. Tulianza vizuri kuliko Arsenal. Lakini ulikuwa ni uamuzi mbaya wa O’Brien kuinua mikono yake. Mambo haya hutokea na wachezaji hawakusudii kufanya hivyo lakini haupaswi kuwa unaweka mikono yako huko juu,” alisema Moyes.

Wapinzani wao wa karibu Manchester City, walipanda kileleni mwa jedwali mapema Jumamosi baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya West Ham United kabla ya mechi dhidi ya Arsenal na Everton.

Erling Halaand alicheka na wavu mara mbili dakika ya tano na 69 naye Tijjani Reijnders akafunga bao moja dakika ya 38 na kuendelea kuganda nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali na alama 37.

Liverpool nao walipata ushindi wa 2-1 dhidi ya Spurs ugani Tottenhan Hotspur. Ugani, St James Park Chelsea walitoka nyuma na kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Newcastle.