Dimba

Muchiri atamba ulengaji shahaba kwa bunduki kuadhimisha Siku ya Wanawake

Na GEOFFREY ANENE March 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MEJA Jenerali Fatuma Ahmed amepongeza klabu ya ulengaji shabaha wa kutumia bunduki ya Pink Target Ladies kwa juhudi za kuunganisha michezo na utendaji wema.

Hii ni baada ya klabu hiyo kuandaa mashindano ya kusherehekea Siku ya wanawake Ulimwenguni katika uwanja wa Kirigiti, Kaunti ya Kiambu, hapo Jumamosi.

Katika mashindano hayo ya siku moja yaliyovutia washiriki 46 kutoka kaunti za Kiambu, Nairobi, Machakos na Mombasa, Kennedy Muchemi alitwaa dhahabu ya kitengo cha Compact Carry Pistol akifuatiwa na Alice Njuguna (fedha) na Hamza Imran (shaba).

Sammy Onyango, Denish Gonzalez na Peter Litiku walifagia nafasi tatu za kwanza kitengo cha Carry Optics. Nao Agatha Muchiri, Druv Shah na Resiato Poreka wakazoa dhahabu, fedha na shaba katika kitengo cha Enhanced Service Pistol katika usanjari huo.

Meja Jenerali Fatuma Ahmed (kushoto) aonyeshwa jinsi ya kulenga shabaha kwa bunduki wakati wa mashindano hayo. PICHA | HISANI

Tatu-bora katika kitengo cha Pistol Caliber Corbine walikuwa Satnam Channa, Elizabeth Cherono na Silvia Kinya, huku Geoffrey Pesa, Joseph Josphat na Husna Ramadhan wakikamata nafasi tatu za kwanza katika kitengo cha Stock Service Pistol, mtawalia.

Charles Mugendi na Adan Mohamed walinyakua dhahabu na fedha katika kitengo cha Speciality Division. Onyango pia aliibuka mshindi wa jumla akifuatiwa na Channa na Mugendi katika usanjari huo.

“Pongezi tele kwa Pink Target Ladies Shooting Club kwa kujitolea kwenu kusaidia shughuli tofauti katika jamii yetu kunatia moyo,” akasema Bi Ahmed.

Aliongeza kuwa mashindano hayo yanaonyesha wazi uwiano mkubwa kati ya mchezo wa ulengaji wa shaba wa kutumia bunduki na wema.

“Jinsi kila ulengaji unahitaji umakinifu na shabaha ndivyo shughuli za uchangiaji katika shughuli za kusaidia. Kwa kuja pamoja hatusherehekei tu ujuzi wetu katika mchezo huu, lakini pia kuonyesha tofauti inayoweza kubadilisha maisha kwa kuchangia sodo ili kusaidia wasichana wanaozihitaji sana katika maeneo ya Kiambu na Ruiru. Mchango huu ni hatua muhimu katika kuwarejeshea heshima, kuwapa elimu na kuwapa uwezo,” akasema Bi Ahmed.