Mwanariadha mkongwe aanza kupokea misaada baada ya kuangaziwa na ‘Taifa Leo’
MWANARIADHA mkongwe wa Kenya, Hezekiah Nyamau ameanza kupokea usaidizi kutoka kwa marafiki baada ya Hali yake kuangaziwa na Kampuni ya Nation Media Group (NMG) inayomiliki gazeti la Taifa Leo.
Nyamau, 88, alikuwa hospitalini kwa zaidi ya wiki tatu kabla ya kuruhusiwa kuondoka Ijumaa wiki jana na anaendelea kupata nafuu nyumbani kijijini Nyaguta, eneobunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii.
Mwanariadha huyo alikuwa miongoni mwa Wakenya wanne walioshinda medali ya dhahabu katika mbio za Olimpiki za Munich mwaka 1972 nchini Ujerumani katika safu ya mita 4×400 kupokezana kijiti.
Wenzake walikuwa Charles Asati, marehemu Robert Ouko na marehemu Julius Sang.
Licha ya kuiletea Kenya heshima, Nyamau alitelekezwa na serikali akiwa hospitalini, na hivyo kuachia familia yake mzigo wa matibabu ya jagina huyo.
Baada ya masaibu yake kuangaziwa na magazeti ya Taifa Leo na Daily Nation, sehemu ya marafiki wa Nyamau kuanzia wiki hii wamekuwa wakimtembelea kumtakia afueni ya haraka.
Mapema wiki hii, Mweka Hazina Msaidizi wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Kenya (NOCK) Charles Mose, Mwenyekiti wa Riadha wa Nyanza Kusini Peter Angwenyi, Mwakilishi wa Wanariadha wa Nyanza Kusini Thomas Osano, na Charles Asati, walizuru nyumbani kwa Nyamau kwake na kumpa msaada wa pesa.
Akizungumza na Taifa Spoti baada ya ziara hiyo, Asati alisema Nyamau alifurahi kuwaona na kuwashukuru kwa kuenda kumuona.
“Alifurahi kutuona. Alitukaribisha kwa uchangamfu. Aliweza kututambua sote kwa urahisi. Aliniambia niketi karibu naye kwa sababu ya wazi ambayo ninyi watu mnajua, nilikuwa mwenzake,” Asati alisema.
Baada ya kina Asati kumzuru Nyamau, Taifa Spoti imefahamu kuwa msaada mwingine kutoka kwa Wizara ya Michezo kwa Nyamau upo njiani.
Aliyekuwa mwanaolimpiki na mshikilizi wa rekodi ya kitaifa katika mbio za mita 400 kuruka viunzi Rose Tata Muya, alisema watamtembelea Nyamau hivi karibuni.
“Ndiyo, tutakuja kumuona. Nitakutana na maafisa wa wizara ya Michezo ili kupanga jinsi ya kumletea zawadi,” Muya alisema.
Alisema kuwa Nyamau atapewa zawadi ya pesa taslimu kama magwiji wengine ambao wamefaidika hapo awali.
“Tunataka kuja ili isionekane kama serikali inampuuza. Alileta heshima kwa nchi hii na lazima tusimame naye anapotuhitaji,” Tata aliongeza.
Mwanaolimpiki huyo wa zamani alibainisha kuwa chini ya utawala wa Rais William Ruto, malipo ya tuzo hizo yalikuwa yameongezwa kutoka Sh300,000 hadi Sh500,000.
Kutokana na umahiri wake katika riadha, Nyamau alijiunga na jeshi la Kenya mwaka wa 1963 na kuhudumu hadi alipostaafu mwaka wa 1997.
Katika mahojiano mengi ya awali na NMG, Nyamau alieleza kukerwa kwake na jinsi serikali ilivyowatelekeza mashujaa na magwiji walioiweka nchi kwenye ramani ya kimataifa katika shughuli za michezo.
Kando na kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki ya 1972, pia alishinda fedha katika hafla hiyo hiyo 1968 huko Mexico.