Dimba

Mwanariadha mkongwe aondoka hospitalini akililia serikali isimsahau

Na WYCLIFFE NYABERI September 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANARIADHA mkongwe Hezekiah Nyamau ameondoka hospitalini alipokuwa amelazwa kwa zaidi ya wiki tatu.

Nyamau, 88, amekuwa akipokea matibabu katika hospitali moja mjini Kisii baada ya kugunduliwa na ugonjwa wa saratani ya kibofu.

Akiwa pamoja na wenzake Charles Asati, wendazao Robert Ouko na Julius Sang, wanne hao waliiletea Kenya sifa kwa kuitwalia medali ya dhahabu katika Olimpiki za Munich, Ujerumani mwaka 1972.

Waliitwaa medali hiyo katika safu ya mita 4×400, kupokezana kijiti.

Kutokana na umahiri wake katika riadha, Nyamau alijiunga na jeshi la Kenya mwaka 1963 na kustaafu mwaka 1997.

Ni baada ya kustaafu kwake ambako mwanariadha huyo alianza kugonjeka.

Katika mahojiano mengi aliyofanyiwa na kampuni ya Nation Media Group, Nyamau alionyesha kutoridhishwa kwake na jinsi serikali ilikuwa imewatelekeza magwiji kama wao na akaomba msaada wa kupigwa jeki maishani.

Taifa Spoti ilimtembelea Nyamau hospitalini alipokuwa amelazwa hivi maajuzi na mwanariadha huyo alitoka kauli fupi lakini ya kuatua moyo.

“Wanangu, kama mwonavyo, sina nguvu za kuwapa mahojiano. Lakini ninawaruhusu mnipige picha ili mwonyeshe Wakenya aliko mwanariadha aliyeletea nchi yetu heshima,” Nyamau aliambia wanahabari wa shirika hili.

Familia yake hata hivyo ilitumia fursa hiyo kuomba msaada kutoka kwa serikali na wahisani wenye nia njema.

“Alipatikana na saratani Februari mwaka huu. Tangu wakati huo, tumekuwa tukiingia na kutoka katika hospitali nyingi kusaka matibabu,” mtoto wa pili wa Nyamau, Pamela, aliambia Taifa Spoti.

Aliendelea, “tumetumia mali nyingi ya familia yetu kwa ajili ya matibabu yake. Ugonjwa huo umemsumbua sana. Ameanza kupoteza kuzungumza kwake. Tunapenda kuchukua fursa hii kuiomba serikali na watu wote wenye mapenzi mema kutuunga mkono pale wanapoweza.”

Mjukuu wa Nyamau, Preston Ondieki alitoa kauli sawia na shangaziye na kueleza matumaini kwamba babu yake atapona hivi karibuni na kurejea katika maisha yake ya kawaida.

“Babu amekuwa mshauri wetu. Tunamtakia kila la kheri na tungependa kumwona akitoka hospitalini haraka iwezekanavyo,” Bw Ondieki alisema.

Nyamau alizaliwa na kukulia katika kijiji cha Nyaguta, eneobunge la Nyaribari Chache, kaunti ya Kisii. Kando na medali ya dhahabu ya Olimpiki ya 1972, pia alishinda fedha katika safu yiyo hiyo kwenye michezo ya 1968 nchini Mexico.

Licha ya kuomba msaada huo, hakuna afisa yeyote kutoka kwa serikali ya kitaifa wala kaunti aliyejitokeza kumfaa katika dhiki. Ni Charles Asati tu, waliyeshinda medali hiyo pamoja aliyekuwa akifika hospitalini humo kumtakia afueni.

Mwenyekiti wa Riadha Nyanza Kusini Peter Angwenyi alidokeza kuwa alikuwa amefahamisha afisi kuu ya riadha na Wizara ya Michezo kwa ujumla kuhusu hali ya mwanariadha huyo mkongwe.

“Nilimweleza Rais wa riadha nchini Bw Jack Tuwei kuhusu hali ya mzee na natumai atasaidika,” Bw Angwenyi alisema huku akitoa wito kwa viongozi kutoka Gusii na Kenya nzima kumsaidia gwiji huyo.

Aliongeza, “tunaomba viongozi hasa wabunge Wetu kuja na kumsaidia Nyamau.”

Kulingana na familia ya Nyamau, mwanariadha huyo aliwaamuru wamwondoe hospitalini na kumpeleka nyumbani.

“Alisema amechoka kukaa hospitalini. Alitueleza tupeleke nyumbani huku akisema yule atakayetaka kumsaidia au kumzuru aje huko,” Pamela alisema.