Dimba

Nimejifunza kuwa mpole tangu nilambishwe sakafu Paris Olympics, akiri nyota Omanyala

Na AYUMBA AYODI October 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala amekiri kuwa kukosa kupata medali kwenye Riadha za Dunia mjini Budapest nchini Hungary mwaka 2023 na Michezo ya Olimpiki mjini Paris, Ufaransa mwaka 2024 kumemfanya aache majitapo.

Omanyala alisema jana kuwa misimu hiyo miwili imemfundisha kuendelea kufanya bidii na kutotosheka kwa sababu kuna ushindani mkali na ukikosea kidogo tu unaishia kujilaumu.

“Ushindani ni kitu kinachokufanya ukose utulivu kwa sababu nadhani kuna wakati nilidhani nimekaa juu ya dunia, lakini nilikashindwa kufika fainali kwenye Olimpiki za Paris,” alisema na kuongeza kuwa yeye huwa hapotezi, lakini anashinda ama kujifunza.

“Siwezi kurudi nyuma na kubadilisha chochote ambacho kimeshafanyika, lakini naweza tu kutumia mafunzo nimepata na kushughulikia vitu vinavyoweza kunifanya niwe bora wakati ujao,” akasema Omanyala.

Hata hivyo, afisa huyo wa polisi aliongeza kuwa lengo lake sasa ni Riadha za Dunia mwaka 2025 mjini Tokyo, Japan ambapo mabingwa wa zamani wa dunia Julius Yego (kurusha mkuki) na Ruth Chepng’etich (marathon) wanatumai kunyakua mataji waliyopoteza.

Omanyala, Yego na Chepng’etich walikuwa wakizungumza wakati wa kuzinduliwa kwa kalenda ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK) ya msimu 2024-2025 inayoitwa “Road to Tokyo”. Shughuli ya uzinduzi iliongozwa na Kati wa Wizara ya Michezo, Peter Tum, na rais wa AK, Jackson Tuwei.

Omanyala alikuwa mmoja wa watimkaji waliopigiwa upatu kutwaa taji la dunia mwaka jana, lakini alisikitisha kumaliza katika nafasi ya saba, huku Mwamerika Noah Lyles akiibuka na ushindi.

Kuelekea Budapest, Omanyala alikuwa ameandikisha historia kwa kuwa Mkenya wa kwanza kushinda mbio za mita 100 kwenye riadha za Diamond League kufuatia ushindi wa duru ya Monaco mnamo Julai 21.

Mwaka huu, Omanyala alipata muda bora duniani wa sekunde 9.79 wakati wa mashindano ya kuchagua timu ya taifa ya Olimpiki mnamo Juni 15, ambao uliimarishwa tu na Kishane Thompson kutoka Jamaica (9.77) mnamo Juni 28.

Hata hivyo, Omanyala, alibanduliwa katika nusu-fainali kwenye Olimpiki mjini Paris baada ya kukamata nafasi ya nane katika kundi lake.

“Mwaka 2024 umekuwa msimu mwingine wa mafunzo…tunajifunza kila siku katika kazi zetu, shuleni na kwa jumla, katika maisha. Hatutawahi kuacha kujifunza,” akasema Omanyala ambaye yuko katika wiki yake ya pili ya likizo.

Omanyala, 28, alifichua kuwa anajaribu kushughulikia masuala ya kibinafsi na pia kuhakikisha wakfu wake wa Omanyala Foundation linafanya kazi kabla ya kutangaza ratiba yake ya msimu mpya mwezi Januari 2024.