Dimba

Nyota Aldrine Kibet asainiwa na Celta Vigo ya Uhispania kwa Sh864 milioni

Na CECIL ODONGO July 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

NYOTA chipukizi wa Kenya Aldrine Kibet amekamilisha uhamisho wake hadi Celta Vigo inayoshiriki Ligi ya Uhispania (La Liga), hatua ambayo inatarajiwa kukweza pakubwa taaluma yake ya soka.

Akithibitisha habari hizo, babake Christopher Komen alisema kijana huyo ambaye anachezea timu ya U20 ya Harambee Stars ametia saini kandarasi ya miaka minne na klabu hiyo kongwe ya Uhispania.

Aldrine sasa anajiunga na Macdonald Mariga na Michael Olunga katika kusakatia timu za Ligi Kuu ya Uhispania.

Habari hizo zimezua msisimko kutoka kwa mashabiki wa soka nchini ambao wamesema nyota ya chipukizi huyo ndio inaanza kung’aa na atafika mbali katika usakataji kabumbu.

Uhamisho wa Kibet unaaminika kugharimu Sh864 milioni na unamweka katika kikoa kimoja na wanasoka wachache kutoka hapa nchini ambao watakuwa wakisakata kwenye ligi za juu za Ulaya.

Kibet aligonga vichwa vya habari mnamo 2023 akiwa nahodha wa St Anthony Boys, Kitale ambapo aliwaongoza kutwaa ubingwa wa soka michezo ya kitaifa ya shule za upili.

Aliibuka Mchezaji Bora na Mfungaji Bora kwenye michezo hiyo iliyoandaliwa Kakamega.

Kufuatia kungáa huko, alielekea Uhispania mnamo 2023 na kujiunga na Akademia ya Nastic Sports ambayo ni ya Gimnastic de Tarragona, timu inayoshiriki ligi ya daraja la tatu Uhispania.

Kutokana na kuendelea kungáa kwake kwenye akademia hiyo, talanta yake ilivutia Celta Vigo ambao sasa wamenasa huduma zake.