Omanyala apokezwa gari la Sh7 milioni na mshirika wake Toyota
KAMPUNI ya CFAO Kenya iliendeleza ushirikiano wake na mshikilizi wa rekodi ya Afrika wa mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala kwa kumpa gari jipya la Toyota Hilux Double Cab linalogharimu Sh7 milioni mnamo Alhamisi, Julai 17, 2025.
CFAO Kenya inasema kuwa gari hilo litasaidia bingwa huyo wa Michezo ya Jumuiya ya Madola katika shughuli zake za kila siku kuelekea mazoezi, mashindano na majukumu mengine.
“Tunajivunia kusaidia Ferdinand Omanyala katika safari yake anapoendelea kupatia taifa na Bara Afrika motisha. Gari hili jipya limejengwa kwa watu wajasiri tu kama Omanyala na linafaa mabingwa wanaohitaji nguvu, starehe na kulitegemea,” akasema Meneja wa Toyota National Sales, Daniel Maundu jijini Nairobi.
Kwa upande wake, Omanyala alisema kuwa kuendesha Hilux kutamsaidia kuimarisha shughuli zake.
“Ni zaidi ya gari tu kwa sababu linanipa uhuru wa kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine, kutafuta matokeo mazuri na kuwakilisha Kenya bila wasiwasi,” akasema Omanyala akifurahia kuendelea kutembea na CFAO Kenya tangu mwaka 2023.