Payet awazia kustaafu soka baada ya tamaa ya sketi kumponza
WIKI chache baada ya kupigwa kalamu na klabu ya Vasco da Gama nchini Brazil, kiungo mahiri raia wa Ufaransa, Dimitri Payet, sasa anawazia kustaafu soka.
Payet, 38, alitimuliwa na waajiri wake kufuatia madai ya unyanyasaji wa kingono dhidi yake.
Nyota huyo wa zamani wa West Ham United alijiunga na Vasco da Gama kwa mkataba wa miaka miwili mnamo Agosti 2023.
Hata hivyo, klabu hiyo iliamua kukatiza kandarasi hiyo na kumweka Payet katika hali ngumu zaidi ya kupata mwajiri mpya baada ya jina lake kupakwa tope.
Waliandika kwenye mitandao ya kijamii: “Vasco da Gama inatangaza kwamba, kwa njia ya kirafiki, imefikia makubaliano ya kusitisha mkataba na kiungo Dimitri Payet mapema.”
“Klabu inamshukuru kwa mchango wake wa kitaaluma, kujitolea kwake na kwa heshima ambayo ameonyesha muda wote huo akiwa Sao Januario, na inamtakia kila la heri.”
Payet alichezea Vasco mechi 77 na akawafungia mabao manane na kuchangia mengine 16. Nyota huyo aligonga vichwa vya habari mnamo Aprili mpenzi wake wa zamani alipodai kuwa alimfanyia ukatili wa “kimwili, kimaadili, kisaikolojia na kingono” wakati wa uchumba wao uliodumu kwa miezi saba.
Mwanasoka huyo alishutumiwa kwa kumlazimisha kipusa Larissa Ferrari kurekodi video za kumdhalilisha.
Ferrari pia alisema Payet alimfanya kushiriki harusi ya uongo na kumvisha pete ya ndoa kwa lazima ili “kuthibitishia ulimwengu mapenzi yao”.
Wakili huyo mwenye umri wa miaka 28 vilevile alidai kuwa Payet alimfanya anywe mkojo wake na maji machafu kutoka chooni, na kulamba sakafu.
Mama huyo wa watoto wawili alisema: “Payet alikuwa katili na mgonjwa wa akili. Alinipiga sana nusura aniue. Nilikuwa nahofia maisha yangu, na bado nina hofu.”
Katika taarifa yake kwa polisi nchini Brazil, Payet alikanusha madai yote ya “unyanyasaji wa kimwili na kisaikolojia” dhidi yake huku akisisitiza kwamba kila kitu kilichofanyika kati yake na Ferrari kilikuwa zao la makubaliano.
Mchezaji huyo ana watoto wanne na mke wake wa karibu miaka 20, Ludivine, ambaye alibaki Ufaransa baada ya Payet kujiunga na Vasco da Gama huko jijini Rio de Janeiro mnamo 2023.
Kabla ya hapo, alikuwa na miaka sita na nusu akichezea Olympique Marseille, akijiunga na timu ya Ufaransa kwa Sh4.4 bilioni kufuatia miezi 18 akiwasakatia West Ham.